Tuesday, October 15, 2013

NAMNA YA KUPUNGUZA MSONGO WA MAWAZO.

Namna ya kupunguza msongo wa mawazo.


-Je una msongo wa mawazo ambao unashindwa kuuepuka? Katika hali ya kawaida ukiushika kwa kuubana mkono wako kwa sekunde kadhaa na kuuachilia, utagundua ni jinsi gani kuubana mkono wako kunavyochosha.
Kushikilia kitu unatumia nguvu nyingi, haijalishi ni nini hasa unachoshikilia kichwani kwako kama ni misukosuko ya mali, kazi, mahusiano yako na watu wako wa karibu katika maisha na mengineyo. Kushikilia au kubeba mzigo huu wa msongo wa mawazo humaliza nguvu nyingi kufikiria ufumbuzi wa matatizo uliyonayo.
‘’Kwanini tusitue mzigo huu wa msongo wa mawazo?’’
Kuna sababu nyingi za mtu kutoepukana na msongo wa mawazo, zikiwemo za kihisia (challenging emotions) na mazingira yanayomzunguka (watu, mali nk).
Mfano;-Unaweza kuogopa kuvunja uhusiano wenu wa kimapenzi na mwenza wako kwasababu unaogopa kuwa mpweke utakapokuacha.
--Unaweza kuogopa kuacha au kufukuzwa kazi kwasababu una wasiwasi wa kukosa kazi mahali pengine hapo baadae au kupata matatizo ya kifedha.
-Swala la msingi hapa ni kujua namna ya kumudu hisia (emotional intelligence) na mawazo yako katika hali ngumu uliyonayo. Huwezi pata jawabu sahihi la matatizo yako mpaka uache kufikiria sana kwanini au imekuaje umepata matatizo yanakusibu na uhamishe mawazo yako katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo uliyonayo. Ninachosisitiza hapa, tumia muda na nguvu nyingi kufikiria suluhu au ufumbuzi wa matatizo yako kuliko matatizo uliyonayo.
Utakapohamisha mawazo yako kwenye kupata ufumbuzi, ni rahisi kufunguka kihisia na kiakili na kupata afadhali katika kupunguza msongo wa mawazo.
-Katika mifano ya matatizo niliyotoa hapo awali ukiwemo wa kuogopa kuachwa na mpenzi wako utaweza kutatua na kupunguza msongo wa mawazo kwa kusema,..’’Naondoa wasiwasi wangu wa kuwa mpweke kwa sasa.’’NenoKWA SASAhusaidia kupunguza msongo wa mawazo kwa wakati huo kwa kukukumbusha kuwa mambo yote hubadilika. Hali ya ukame ya sasa haimanishi itadumu mpaka masika.
Kubadilika ni swala la kibinadamu, mtu huweza kubadilika kila mara kulingana na msukumo wa ndani yake (hisia na akili zake) au shinikizo la kimazingira yanayomzunguka. Kwa kawaida mtu mwenye kushikilia sana matatizo yake sana kiakili hufanya mambo kuwa magumu zaidi kuliko yule aliyeamua kutua mzigo wa msongo wa mawazo.
Ushauri wa namna ya kupunguza msongo wa mawazo.
-Kama tatizo lako ni kubwa, jaribu kutatua shida ndogondogo kwanza hatimaye kumalizia na shidailiyokubwa.
-Kubali kutua mzigo wa msongo wa mawazo kwa kuacha kubeba na kushikilia kichwani mambo ambayo yapo nje ya uwezo wako. Utakapofanya hivyo ni kama kitendo cha kuhema, unatoa hewa chafu nje na kuvuta hewa safi ya uzima ndani. Kwa kufanya hivyo unapumzisha akili.
-Kama tatizo lako ni dogo tu labda mtu amekuudhi au umeshindwa kabisa kumudu hisia zako na mawazo yako ni heri kwenda mahali penye watu wengi penye starehe ya aina fulani kama labda ni beach, cinema au mahali pa kukufanya ujiliwaze na kupunguza mawazo yako. Kwenda mahali penye watu wengi ni muhimu pia kwasababu unapokuwa katika sehemu yenye watu wengi ni rahisi kusaidiwa na watu wanaokuzunguka iwapo utataka kufanya jambo la ajabu kwasababu ya mawazo au hasira ulizonazo.
-Ikiwa hupati majibu kwa yale mambo yanayokufanya uwaze sana, tafuta ndugu, jamaa au rafiki yako wa karibu sana unayemuamini na umueleze matatizo yanayokusibu huenda ukapata ushauri au njia mbadala ya kutatua matatizo yako.
-Pima uzito wa mambo yanayokupa mawazo tele, kama jambo hilo sio la msingi sana katika maisha yako unaweza kuupuza na usilipe nafasi katika akili yako. Mawazo mengi yasiyo ya kukujenga kimaisha au mawazo yasiyo na tija ni vyema ukayapuuza ili kuondekana na msongo wa mawazo usio wa lazima. Akili yako ina mambo mengi ya kufikiri, ijaze na mambo mazuri yatakayokusaidia sasa na hapo baadae. Usiijaze na sumu kama hasira, mawazo potofu na mambo mengine yatakayoweza kukubomoa.
Kama una chochote cha kuongeza kuhusiana na mada hapo juu, tafadhali usisite kutoa maoni yako!

No comments:

Post a Comment