Tuesday, October 15, 2013

MAGONJWA NYEMELEZI NA DALILI ZAKE.(toleo la pili)

Mkanda wa jeshi.
Husababishwa na kirusi kiitwachoVaricella Zoster (VSV).Mara nyingi hutokana na kuamshwa kwa ugonjwa ambao ulikuwepo mwilini hapo awali (reactivation of an earlier infection).Mbali ya kuathiri ‘uwanda’ (dermatome) moja au zaidi wa mishipa ya fahamu (neva), pia huweza kudhuru jicho (herpes zoster opthalmicus) na sikio (herpes zoster oticus).
Dalili zake ni maumivu makali katika ‘uwanda’ ulioathirika, homa, vipele, maumivu ya kichwa, uchovu na maumivu ya macho kutokana na mwanga (photophobia).
Maumivu ya Retina
Kwa lugha ya kitaalamu huitwa CMV Retinitis na husababishwa na kirusi kiitwacho Cytomegalovirus (CMV). Kirusi hiki, mbali ya kuathiri jicho na haswa retina, pia huathiri viungo vingine kama mapafu na kusababisha nimonia, utumbo mpana na mfumo wa fahamu ambako husababisha maumivu.
Dalili zake ni pamoja na kutoona vizuri, macho kuuma, kutokwa na machozi kwa wingi.Kutopata matibabu mapema huweza kusababisha upofu.Pia Huweza kuathiri viungo vingine na kusababisha homa, nimonia, kichefuchefu, kuharisha na kupungua uzito.
Magonjwa yatokanayo na Fangasi.
Fangasi pia huweza kujitokeza iwapo kinga ya mwili itashuka.
Kandidiasisi.
Ugonjwa huu uliozoeleka pia hujulikana kwa kitaalamu kama Candidiasis. Kandidiasisi husababishwa na fangasi aitwayeCandida albicansambaye huathiri kinywa, mfumo wa chakula,uke na mfumo wa hewa.Kandidiasisi katika uke huweza tokea kwa mwanamke mwenye afya asiye na VVU.
Dalili za Kandidiasisi katika kinywa ni pamoja na kubadilika kwa ladha, maumivu kwenye ulimi, utando mweupe kwenye ulimi na kingo za juu za kinywa (buccal mucosa), kushindwa kumeza ,maumivu wakati wa kumeza chakula ikiwa fangasi imesambaa sana. Pia mwasho na maumivu ukeni pamoja na kutokwa na majimaji meupe ukeni.
Homa ya Uti wa mgongo.
Homa ya uti wa mgongo au Meningitis kwa kitaalamu husababishwa na fangasi aitwayeCryptococcal neoformans. Uti wa mgongo utokanao na aina hii ya fangasi huweza kusababisha kifo usipotibiwa. Aina hii ya fangasi ambayo huathiri zaidi ubongo na uti wa mgongo, hutokana na kuvuta hewa yenye vumbi litokanalo na ndege lenye vimelea vya ugonjwa.
Baadhi ya dalili zake ni homa, kutoona vizuri, macho kuuma kutokana na mwanga, kuchanganyikiwa akili, maumivu ya kichwa ka kukakamaa na kuuma kwa shingo.
Histoplasmosisi.
Aina hi ya fangasi hutokana na vimelea vyaHistoplasma capsulatum. Fangasi huyu huathiri mapafu pamoja na viungo vingine. Dalili zake ni homa,uchovu,kupungua uzito na kupumua kwa shida. Pia kukohoa na kuvimba kwa tezi kwaweza kutokea.
Nimonia.
Kama bakteria na fangasi pia huweza kusababisha nimonia ijulikanayo kwa kitaalamu kama Pneoumocystis Pneumonia (PCP). Vimelea vya Pneumocystis jiroveci (awali vilijulikana kama Pneuomocystis carinii) huathiri mfumo wa hewa. Fangasi huyu pia huweza kuathiri viungo vingine kama ini, wengu (spleen) na figo katika baadhi ya wagonjwa.
Dalili zake ni kikohozi kikavu,kifua kubana,kupumua kwa shida,homa,kuishiwa pumzi na kutokwa jasho nyakati za usiku.
Magonjwa yatokanayo na Protozoa.
Toksoplasmosisi ya Ubongo.
Cerebral toxoplasmosis, kama ujulikanavyo kitaalamu, hutokana na kuamshwa kwa ugonjwa wa awali kutokana na vimelea vyaToxoplasma gondii(kimelea kiwezacho kuishi ndani ya seli kinachoathiri ndege, wanyama na binadamu). Kimelea hiki kiathiricho zaidi mfumo wa fahamu hupatikana kwenye nyama isiyopikwa vizuri na kinyesi cha paka. Huathiri zaidi ubongo na kusababisha maumivu ya kichwa, kuchanganyikiwa, udhaifu wa viungo, homa, kupoteza fahamu, kupooza na kifafa.
Kriptosporidiosisi.
Huu ni ugonjwa utokanao na vimelea vyaCryptosporidium. Huathiri zaidi mfumo wa chakula na hutokana na kutumia kwa maji au chakula vilivyoathirika na vimelea vya ugonjwa huu. Dalili zake ni kuharisha sana kiasi cha kusababisha kupungukiwa na maji mwilini (dehydration), maumivu wakati wa haja kubwa, kichefuchefu na kutapika. Wagonjwa wa aina hii huwa na joto la mwili la kawaida.
MATIBABU NA USHAURI.
Aina ya matibabu hutegemea na aina ya ugonjwa na mtu, pia kutokana na kuwepo kwa Ukimwi/VVU hutegemea kiwango cha seli za CD4 mwilini. Iwapo una dalili kati ya zilizotajwa hapo juu ni vyema kumuona daktari kwa uchunguzi zaidi.
Kuwepo kwa dalili zilizotajwa hapo juu hakumanishi kuwa mgonjwa ana VVU na si kila mwenye VVU huwa na dalili hizo. Pia kujitokeza kwa dalili kunaweza kutofautiana kati ya mtu na mtu. Hata hivyo ni vyema kupima afya yako kila mara haswa VVU ili kujua chanzo cha kupungua kwa kinga ya mwili ambayo huweza kupelekea kupata magonjwa nyemelezi.
NAKUTAKIA AFYA NJEMA NA MAFANIKIO TELE KATIKA MAISHA YAKO.
Kama una chochote cha kuongeza kuhusiana na mada hapo juu, tafadhali usisite kutoa maoni yako!

No comments:

Post a Comment