Saturday, March 8, 2014

Njia 19 za kukufanya uonekane unajiamini.

Kujiamini kwako kutakufanya uonekane wewe ni mwanaume au mwanamke mwenye uhakika na mahiri katika kazi zako. Licha ya hivyo ikiwa utapendeza kwa kuvaa vizuri yani kuwa maridadi na nadhimu utaonekana unajipenda na mwenye utashi wa kufanya vyema katika shughuli zako au jambo lolote lile. Kila mtu huvutiwa na kujiamini kwa mtu katika mambo yake hivyo ikiwa nawe unataka uonekane unajiamini soma hizi njia 19 zikusaidie kuongeza wasifu wako wa kujiamini. 1. Jijengee mazoea ya kuongea kwa sauti kubwa ya kusikika vizuri na epuka kutamka maneno vibaya. 2. Unapokuwa umesimama simama wima, usiweke mikono mfukoni na pia usijiegemeze kwenye kitu kingine mfano meza, ukuta, nguzo nakadhalika. 3. Unapoongea na mtu jipe nafasi ya kutosha kwa kuwa karibu na mtu unayeongea naye bila kumsogelea sana, yatawale mazingira yako. Tumia mikono yako kuelewesha kile unachokisema. Kama umekaa kwenye kiti basi kaa kistaarabu, pia unaweza weka miguu yako mkao wa kukunja nne lakini chunga usijilegeze na kuonekana umejitandaza. 4. Wakati wote jitahidi kutulia bila kujionyesha una wasiwasi. Ondoa wasiwasi unaoweza kukufanya usikae mahali kwa amani. Tulia bila kuhofia kitu chochote, pumua taratibu na utajisikia vizuri mapigo yako ya moyo yatakuwa sawa na mwili wako utapata nguvu. 5. Unapoongea na mtu muangalie machoni kwa kuonyesha uso wa bashasha. Kuwa makini kumsikiliza na tikisa kichwa pale unapoafiki anachokuambia kama ishara ya kuwa unampata na kuelewa anachokwambia lakini usimkodolee macho sana. Unaweza pepesa macho pembeni lakini isiwe mara nyingi sana kuonekana husikilizi au una aibu. 6. Jiheshimu na jithamini uwe mtu wa kuheshimiwa. Watu watakuchukulia kwa namna utakavyojiweka. Kwa kadri utakavyojiheshimu na kujiona wewe yu jasiri ndivyo watu pia watakavyokuona. 7. Unapotaka kuangalia pembeni, zungusha kichwa upande kuelekea mahali unapotaka kutazama bila kujigeuza mwili mzima. Tazama bila kupepesa macho sana kuonekana unahofia kitu fulani. 8. Jitahidi sana kuwa mwenyewe, usitake kuigiza mtu mwingine anachofanya. Unaweza kujifanya kama mtu fulani kwa muda ikiwa tu unataka kujifunza kujiamini na kuwa kama yeye. Lakini utakapokuwa umeshajenga ujasiri ni vizuri ujiongoze mwenyewe kwa kufanya mazoezi zaidi ya kuongeza ujasiri wako. (Mfano kwa kuongea mbele ya umati wa watu, kujieleza na kumshawishi mtu afanye unalotaka nk) 9. Kama unategemea kuwasilisha ujumbe kwenye mhadhara au mkutano (kwa maana ya kufanya presentation) jiandae vyema na mapema kabisa hasa pale presentation inapokuhitaji uwe na notes au muongozo wa nini unatakiwa uwasilishe ili kuepusha kutoweza kusoma na kutamka baadhi ya maneno vizuri. 10. Vuta pumzi kila unapokuwa na hofu ya kushindwa kufanya kitu fulani kisha jiambie "NAWEZA" kisha fanya kitu hicho bila kufikiria kuwa utashindwa. 11. Fanya mambo yako kwa umakini na jiamini kuwa kila kitu kitakwenda vizuri, kwa kufanya hivyo utaonekana kwa watu unajiamini kwa kile unachoweza kufanya. Ni vizuri kujenga hisia za ujasiri ndani yako kuwa UNAWEZA kufanya lolote bila uwoga. 13. Unapokuwa unaongea na kuhisi sauti yako haitoki vizuri, kunywa maji kama unadhani mate yatakuwa yamekukauka na rekebisha koo kisha hesabu 1, 2, 3 mpaka 20 kwa kupaza sauti kwa kadri unavyokaribia kufika ishirini. 14. Unapoongea na mtu/watu zaidi ya wawili, jitahidi kumiliki ujumbe wako kwa kueleza vizuri kile unachosema. Kama hutoweza kusema vizuri ni rahisi mtu mwingine kukusaidia kuelezea hivyo utaonekeana hujajipanga. Jipange vizuri kwa kujua nini unataka kuongea kabla ya kuanza kuzungumza. 15. Ongea kwa kutamka maneno vizuri bila kwenda mbio na jitahidi kutoongea sana. Ongea kwa kiasi kisha tulia kwa sekunde kisha endelea. Hakuna sababu ya kutaka kuongea mengi bila kusimama lengo ni ujumbe ufike kwa wale wanaokusikiliza. Ukiongea kwa haraka utaonekana hufahamu vizuri unachokisema hivyo unataka kumaliza haraka. 16. Onyesha kujipenda kwa kutabasamu au kucheka kila unapofurahishwa na jambo fulani. Amini usiamini tabasamu humfanya mtu aonekane hana wasiwasi wowote kwa kuwa anajiamini. 17. Unapoongea unaweza pia kutumia misemo iliyowahi kusemwa na watu wengine kuhusiana na mada mnayoongelea ili kuongeza msisitizo wa kile mnachokiongelea. 18. Unaposhindwa na jambo jitahidi kutokuonyesha umejisikia vibaya kushindwa. Kukunja sura kwa huzuni au kwa kukasirika baada ya kushindwa jambo fulani kutakufanya uonekane umefadhaishwa na aibu. 19. Ni muhimu kuonyesha uaminifu na uadilifu wako kwa watu. Kujiamini kunaendana na kuaminika. Ukiwa unajiamini halafu huna maana kwa watu ni sawa na kujigamba pasipo kuwa na lolote la kujivunia. Jisikie kuwa wewe ni jasiri na mwingi wa furaha, onyesha uungwana wako kwa watu nao watakuthamini. Kama unachochote cha kuongeza kuhusiana na mada hapo juu, tafadhali usisite kutoa maoni yako!

No comments:

Post a Comment