Sunday, November 10, 2013

Namna ya kupunguza matumizi ya fedha.

Namna ya kupunguza matumizi ya fedha.
Kujua kiasi gani unachoingiza mfukoni kwa siku na jinsi unavyotumia pesa zako ni swala muhimu sana. Ukitaka kujua umuhimu wa kutunza akiba ya fedha unazochuma kwa matumizi yako ya baadae ni pale unapoishiwa pesa kabisa na kushindwa kujikimu. Hapa ndipo mtu huyo aliyeishiwa kama asipotumia busara katika kutafuta njia sahihi na mbadala za kumwezesha kuondokana na hali yake ya kutokuwa na pesa huzaa matatizo mengine kama kuwa na madeni lukuki, kuuza mali zake ili afiidie kupata mahitaji yake mengine muhimu nakadhalika. Hizi ni bakshishi za kukusaidia ufanye matumizi mazuri ya fedha zako kama ifuatavyo.
1. Tunza kumbukumbu ya matumizi yako makubwa ya lazima unayotumia.
-Matumizi muhimu unayotumia nyumbani ni kama umeme, maji, gesi kwaajili ya jiko, mafuta ya gari au pikipiki unayotumia kwenda kazini au sehemu mbalimbali na mahitaji yako mengine ya kila siku. Ni muhimu ujue matumizi yako ya siku ili ufahamu ni kwa namna gani utatumia pesa yako, ukiwa na kumbukumbu ya matumizi yako ni rahisi kujua kama unaendelea na matumizi mazuri au umezidi kutumia pesa kuliko kiwango cha pesa unachoingiza.
2. Punguza matumizi ambayo siyo ya lazima.
-Hii ni sababu kubwa ya watu kulalamika kuwa hawajui pesa zao zinapotelea wapi lakini ukichunguza kiundani utagundua watu wengi huwa tunanua vitu vingi sana ambavyo sio vya lazima kuliko vile muhimu ambavyo hatuna budi kuwa navyo. Nunua vitu kwa sababu sahihi kwa matumizi yako.
3. Unapokwenda kufanya ununuzi wa vitu mbalimbali, tengeneza orodha ya vitu unavyotaka kwenda kununua.
-Kuwa na orodha ya vitu unavyokwenda kununua kama ni supermarket au sokoni. Kwa kufanya hivyo utaepusha kutokununua vitu ambavyo hukupanga kuvinunua hapo kabla. Angalizo usiende supermarket au sehemu yeyote ambapo wanauza vyakula ukiwa unahisi njaa maana utapokwenda ukiwa na njaa unaweza kutamani vyakula na vitu vingine vingi ambavyo hukutegemea kuvinunua.
4. Kuwa na mpango mzuri wa kutumia pesa zako kwa kuwa na bajeti.
-Bajeti ndio mpango mzima wa matumizi yako kulingana na kiasi cha pesa ulichonacho, bajeti hukuonyesha kikomo cha matumizi yako hivyo hukusaidia kutumia pesa zako kwa mpango mzuri. Kama hutakuwa na bajeti ni rahisi kwako kutumia pesa kupita kiwango chako cha utafutaji na kupata matatizo ya kuwa na uchumi mbaya hapo baadae.
5. Kama una madeni tafuta namna ya kuyapunguza kidogokidogo.
-Hakuna kitu kinachomrudisha mtu nyuma kimaendeleo kama madeni yaliyokithiri, kuwa na madeni yatokanayo na mkopo au sababu nyingine ni sawa lakini pale mtu anapokuwa nayo mengi kufikia kushindwa kulipa hapo ndipo pabaya. Kopa kwa malengo na mipango mizuri itakayokuwezesha utumie pesa ulizokopeshwa kwa maana nzuri yenye tija. Ni vizuri pia uwaone washauri pamoja na watu wengine wakushauri kuhusu mikopo kabla ya kwenda kuchukua kukopa.
6. Punguza kuweka vocha kwenye simu kwaajili ya maongezi ambayo sio ya lazima.
-Hasa sisi vijana kwa kuchati na kuongea na simu sana ndio kawaida yetu lakini swali linakuja,je ni kweli mazungumzo yote huwa ni yenye ulazima kwetu. Kwa kawaida dakika 3 za kwanza za maongezi huwa ni zenye kutumika vizuri sana kwa kuwa utaongea mambo yote muhimu unayotaka kuongea lakini baada ya hapo maongezi zaidi sidhani kama ni yenye umuhimu. Haya labda umejiunga na huduma za promosheni na kupata SMS au dakika za bure ambazo umeshazilipia na kutumia muda mwingi kuongea, licha ya kupoteza pesa kila siku bali pia unapoteza muda kila siku kwaajili ya kuchat na kuongea na simu pasipo kuwa na tija.
7. Kama una fedha kiasi cha ziada, fungua savings account.
-Ukiwa unaingiza kiasi kikubwa cha fedha za matumizi na kupata pesa za ziada, jijengee tabia ya kuhifadhi angalau asilimia 10 au 20 ya kiasi cha fedha unachoingiza. Pesa zako utakazohifadhi zitakusaidia baadae utapokuwa na uhitaji nazo.

1 comment: