Friday, January 3, 2014

Faida saba (7) za kupenda kujisomea sehemu ya pili.



5. Kusoma kunaongeza ujuzi wa kuandika vizuri.
Ukiwa unasoma kila siku kwa walau dakika chache (dakika 15-30) tu iwe ni gazeti au jarida la habari, kitabu au kurasa kadhaa za tovuti mbalimbali kwenye intaneti, basi kuna uwezekano mkubwa wa kuwa umesoma na kuona mengi. Unaposoma sana ndivyo unavyoongeza ujuzi wako katika kupangilia na kuandika maneno vizuri. Makala nyingi tunazosoma kwenye magazeti na tovuti za kuaminika kwenye mtandao wa intaneti zinakuwa zimeandikwa na waandishi au watunzi mahiri katika sanaa ya uandishi. Hivyo unaposoma kazi zao unajifunza mengi kuhusu namna ya kuandika na kupanga kazi zako za kimaandishi vizuri.
6. Kusoma kunapunguza msongo wa mawazo.
Inaaminika kusoma kunaweza kukuchangamsha kwa kuhamisha mawazo yako kabisa na kufuatilia kile unachosoma kwenye kitabu kwa wakati huo. Mfano: Hebu chukua jarida la vichekesho, mkasa wa maisha wenye kukupa hamasa au kitabu takatifu cha kiimani (BIBLIA au QURAN TUKUFU). Kwa kadri utakavyokuwa unasoma na kujifariji ndivyo unavyokuwa unatuliza akili na kuwa katika hali ya amani na utulivu wa nafsi. Utakavyokuwa na utulivu wa nafsi na akili ndivyo utakavyokuwa na afya njema kwa kuondokana na maradhi kama ya kuathirika kisaikolojia, shinikizo la damu (blood pressure) nakadhalika.
7. Kusoma kuna burudisha.
Inafurahisha sana kumkuta mtu anasoma gazeti akicheka kwa kuwa amefurahisha na kile anachosoma. Hadithi za kwenye vitabu, mashairi na vibonzo (katuni) vya magazetini na majarida mbalimbali ni baadhi tu ya viburudisho unavyoweza kusoma na kufurahi. Ulimwengu wa vitabu una mengi ya kusoma, kujifunza na kuburudika kazi ni kwako.

No comments:

Post a Comment