Namna ya kufanya siku yako kuwa nzuri.
Kuwa na siku nzuri itatagemea wewe mwenyewe mambo gani utafanya kwa siku hiyo kama ni kazi au shughuli zako za kila siku za nyumbani, kazini, shuleni au popote pale ulipopanga kuwa kwa siku hiyo. Kwa namna utakavyotumia siku yako kuanzia umeamka asubuhi na mapema mpaka kufikia jioni ndio kitu cha msingi sana cha kutathmini kila siku.
Ni vizuri kutathmini yale yote uliyofanya kwa siku kwa kujiuliza mwenyewe kama siku yako ilikuwa ni yenye faida au hasara.MwanafasafaJim Rohnaliwahi kusema
“At the end of the each day, you should play back the tapes of your performance. The results should either applaud you of prod you.”– Jim Rohn
Kwa maana hiyo ikiwa kila mwisho wa siku utatumia walau dakika 10 kutathmini yale uliyofanya na kupima matokeo ya yale uliyofanya kwa siku lahasha utakuwa umefanya jambo la msingi litakalokuwezesha kutambua udhaifu na uhodari wako, faida na hasara uliyopata kwa siku. Unaweza kujiuliza hivi,
*.Je siku yako ilikuwa nzuri au mbaya ?
*.Umefanya nini kwa siku ya leo kilichokupa faraja?
*.Je leo umekasirika? Kama NDIYO ni nini kilichokuchukiza?
*.Umefanya jambo gani zuri lililokupa faida kwa siku ya leo?Faida inaweza kuwa ni umeimarisha mahusiano yako ya kimapenzi na wako umpendae, umeonyesha upendo wako kwa ndugu au familia yako, inaweza kuwa umejiingizia kipato kikubwa cha fedha kutokana na kazi au biashara yako, umekwenda kliniki ku-check afya yako, umechangia kununua kitu fulani nyumbani kwa manufaa ya familia yako nakadhalika. Ninachomaanisha hapa ni kujitahidi angalau kila siku uwekeze kitu kidogo cha kimaendeleo sio lazima iwe ni pesa au mali bali kinaweza kuwa kitu chochote kile.
Inapendeza sana ikiwa mtu atatumia siku yake vilivyo kufanya yale yote yanayomletea faraja na kumfanya aishi maisha yenye mantiki kwake na hatimaye kufanikiwa kila siku katika yale aliyoazimia kufanya kwa siku hiyo.
Kujua zaidi: Soma Maswali muhimu ya kujiuliza kila siku.
Soma haya mambo saba (7) yakusaidie siku yako kuwa nzuri.
1. Kuwa na fikra chanya kwa kuwaza mema.
Ifanye akili yako ifikiri kila kitu kinawezekana, jiamini na fanya mambo yako kwa umakini na uhodari ukijua kila kitu kitakwenda vizuri.
2. Fanya mazoezi kuweka mwili wako sawa.
Amka asubuhi na mapema saa 11 au 12 asubuhi, fanya mazoezi angalau kwa dakika 30. Nyoosha viungo vyako vya mwili, ukitokwa na jasho jipongeze kwa kuwa ni kipimo cha kuwa umejishughulisha kufanya mazoezi ipasavyo. Kunywa maji kupooza mwili, pata juisi fresh ya matunda kisha endelea na shughuli zako nyingine.
Unaweza soma pia: Je unajua manufaa ya kufanya mazoezi?
3. Kula vizuri.
Usijaze tumbo lako kwa kula vyakula vibaya. Epuka kula vyakula vyenye mafuta mengi, chumvi au sukari nyingi. Kula wanga kiasi, ni vizuri pia kunywa supu au mchemsho wa nyama (ng’ombe, kuku, bata, samaki n.k), usisahau pia katika mlo wako kuwa na mboga mboga za majani na matunda. Kula vizuri kwa afya bora.
4. Ondoa hofu au wasiwasi.
Kuwa na amani pamoja na utulivu wa nafsi. Hakuna sababu ya kuhofia kitu kwakuwa mara nyingi unavyohofia huwa si vya kweli au hata kama ni vya kweli ni kwa nadra sana vitakutokea kwako. Jifunze kuona sio kila kitu kinachowatokea wengine nawe lazima vikupate. Upe faraja moyo wako na kuwa na matumaini kwa kutegemea mambo mazuri yanakuja mbeleni hata kama si leo basi ni kesho. Usikate tamaa kwa shida ya leo iliyokufanya ufadhaike na kuhofia kesho kuwa hali itakuwa mbaya zaidi.HAPANAsiku hazigandi ya jana si lazima yawe ya leo. Inuka kwa ujasiri, jifunze kutokana na makosa yaliyokufanya ujikwae na songa mbele.
5. Jifunze kitu kipya kila siku.
Soma lolote linaloweza kukujenga kimaisha kwa siku ya leo. Wewe ni mfanyakazi basi soma kitu chochote cha kukuongezea ujuzi kwenye kazi yako na kupanua wigo wa kuendeleza, kukuza na kuboresha kazi yako kuwa bora zaidi. Ama kama wewe ni kijana wa nyumbani huendi shule au hufanyi kazi yeyote ile ya ziada zaidi ya hizo za nyumbani, tafuta mahali popote karibu na nyumbani wanapotoa mafunzo yeyote ya stadi za kazi, ujasiriamali au elimu yeyote ile ya maisha. (Jifunze ufundi wa kujenga nyumba, kushona nguo, kilimo, ufundi seremala, mapishi nakadhalika). Noa maarifa yako kwa kuongeza ujuzi.
6. Tabasamu au cheka kwa furaha kila unapofurahishwa.
Huna sababu ya kununa wakati wote, tabasamu kama mtoto mchanga asiyejua shida yeyote. Furahia kila wakati mzuri unaopata kuwa na rafiki, ndugu, jamaa au familia yako. Furaha yako ni tiba nzuri kwa afya yako kwakuwa unajiepushia matatizo mengi kama msongo wa mawazo (stress), shinikizo la damu (blood pressure) nakadhalika. Ishi kwa wakati bila kujiwekea kisirani cha mambo ya jana au yaliyopita.
7. Jipumzishe kwa kulala vizuri.
Lala usingizi mzuri wenye utulivu na amani kwa masaa 8. Ikiwa utakuwa busy sana basi jipumzishe kwa kulala angalau masaa 6. Zingatia ubora wa usingizi (lala mahali safi, tulivu na pasipo na adha yeyote ile) na si bora kulala tu. Lala usingizi mzuri kwa afya bora.
No comments:
Post a Comment