Thursday, December 5, 2013

JINSI YA KUDHIBITI HASIRA.

Jinsi ya kudhibiti hasira.

Kila mtu hukasirika pale anapochukizwa au kukasirishwa na jambo fulani, hali hii humtokea mtu yeyote. Ikiwa utaruhusu hasira zikutawale zitakupelekea kuvuruga akili yako na hatimaye kudhohofisha afya yako. Hasira sio kitu kizuri kabisa, hasira inaweza kuwa ni ya kubomoa au kujenga lakini mara nyingi hasira husababisha hasara kwa kuwa inabomoa na kuharibu mambo. Hebu tuangalie hii mifano miwili; *.Unaingia nyumbani na kukuta sebuleni kumekaa hovyo makochi, meza na vitu vingine vimekaa shagara bagara. Unakasirika na kuona vitu vimekaa vibaya na kuamua kupanga na kuweka kila kitu sawa. Baada ya muda sebule inaonekana ni yenye kupendeza tena. *.Mzazi wako anaongea na wewe na kukuomba umueleze kwanini umechelewa kurudi nyumbani. Unakasirika na kuamua kumfokea hadi kutaka kupigana. Baada ya muda mzazi wako anachukizwa kwa kile ulichofanya na wote mnakuwa katika hali mbaya ya kutoelewana. Katika mifano hiyo miwili hapo juu tunaona ni jinsi gani hasira inaweza kukujenga na kukufanya ufanye jambo kwa ari na kwa nguvu zako zote vilevile hasira inaweza kuharibu mambo na kukupelekea uwe katika hali ya majuto. Kwa kujua hayo hizi hapa ni mbinu za kukusaidia kutuliza hasira zako. 1. Fikiri kabla hujaongea. -Unapojihisi unashindwa kujitawala na kupandisha hasira. Ni vyema ukakaa kimya au kuondoka kabisa mahali ulipo ili kuepusha shari au kuongea mambo ambayo yatakufanya ujute hapo baadae. Utakaponyamaza ni rahisi hata kwa mtu/watu unaongea nao kutulia kwakuwa hutoonyesha dalili ya kutaka kujibishana. Ikiwa mtu atakulazimisha kwa namna moja au nyingine uongee basi ni vyema ukamwambia sipo tayari kuongea kwa sasa labda baadae na ondoka katika eneo hilo bila kusema neno lingine lolote. 2. Vuta pumzi. -Unapopandisha hasira, mapigo yako ya moyo yanaongezeka kwa kasi, nguvu nazo zinaongezeka na mwili wako unakuwa tayari kufanya lolote pasipo kufikiri na kushindwa kujitawala. Kufikia hatua hiyo ni hali mbaya sana inayoweza kukupelekea kufanya jambo lolote la hatari. Hali hiyo inapaswa kudhibitiwa na wewe mwenyewe kabla hujakuwa na hasira zaidi. Itakubidi ushushe hasira zako kwa kukaa chini na kutulia kisha vuta pumzi, jitahidi kuhimili mihemko yako ya mwili kwa kutofanya lolote bali kutulia na kuvuta pumzi na kupumia angalau kwa dakika 5. Vuta pumzi ndani taratibu na kwa wingi kisha pumua. Baada ya dakika 2-3 bila shaka utaanza kujisikia mwenye amani. 3. Nenda mahali penye amani au popote penye kuleta furaha. -Ukiwa na hasira iliyokutawala kwa muda mrefu ni vizuri kwenda mahali ambapo unaweza kupata furaha mfano kwenye fukwe za bahari au ziwa (beach), bustani nzuri yenye majani na maua ya kupendeza au mahali ambapo kuna mkusanyiko wa watu wengi na shughuli za kijamii zinafanyika kama kwenye stadium (uwanja wa mpira wa miguu, kikapu, nyavu n.k) na pengine popote pale ambapo unaweza ukaondoa mawazo mabaya na kujifariji. 4. Hesabu namba kichwani 1 mpaka 20. -Unaweza kuona mbinu hii ya kuhesabu namba kama haina maana lakini ikiwa utaitumia itakusaidia kuondoa mawazo ya kitu au mtu aliyekukasirisha na kuweza kujimudu kupambana na hasira zako. Vuta pumzi na kisha pumua taratibu, anza kuhesabu namba kuanzia 1 kupanda mpaka 20 bila kufikiri chochote isipokuwa weka mawazo yako katika kuhesabu namba. Usiruhusu mtu akukatishe hivyo itabidi ukae mahali peke yako au ikiwezekana tulia na hesabu namba zako bila kusikiliza chochote kingine. 5. Eleza shida yako au kitu kinachokukera kwa mtu wako wa karibu unayemuamini. -Kueleza mambo yanayokusibu kwa mtu ni njia nzuri ya kutoa kero zako zinazokufanya ukasirike. Mtu wako wa karibu anaweza kuwa mzazi, shangazi, kaka au jamaa yako. Ikiwa utaeleza kero zako kwa mtu wako wa karibu utatoa yaliyo moyoni mwako na kuwa mwenye amani. Pia utakapomueleza mtu yanayokusibu ni rahisi kupata ushauri mzuri kutoka kwake ambao huenda utakusaidia kutatua tatizo lako. 6. Epuka kuwa karibu na mtu au kitu kinachokuchukiza. -Unaweza kuwa unakasirika kila umuonapo mtu fulani usiyempenda, pia unaweza kuwa unakasirika kila uonapo kitu fulani usichokipenda. Chochote kinachokufanya ukasirike ni vyema ukakiepuka ili usichukie. Kama ni mtu fulani ndiye anakusababisha ukasirike ni vyema ukatafuta ufumbuzi wa mgogoro wenu na kuweka mambo sawa. 7. Fanya zoezi lolote la kuchangamsha mwili. -Jishughulishe na mchezo wowote au mazoezi kama kuogelea, kuendesha baiskeli, kukimbia angalau kilomita 2 au tembea kwa miguu. Lengo ni kubadilisha mazingira, kufikiri na kuona mengine kuliko kukaa sehemu moja na kufikiri mambo hayo hayo yanayokusabibisha upate hasira.

No comments:

Post a Comment