Tikitimaji ni tunda lenye ladha nzuri na tamu sana. Lina maji kwa 92% na sukari kwa takriban 6%. Licha ya kuwa juisi ya tikitimaji au tunda lenyewe hukata kiu kwa haraka bado kuna faida nyingine nyingi za kiafya tunazonufaika kutokana na tunda hili. Je ulikuwa ukijua tikitimaji lina sukari asilia yenye kukupatia nguvu mwilini, vitamin A, C, E, D, niacin na madini kama ya chuma (iron), calcium, magnesium, manganese, potassium, phosphorus, zinc nakadhalika. Faida nyingine ya tunda hili ni kwamba halina mafuta kabisa hivyo ukila tikitimaji huwezi kuongeza mafuta au cholesterol mwilini.
Angalia hii video hapa chini yenye maelezo ya namna ya kutengeneza juisi ya tikitimaji na faida za tunda lenyewe.
Hebu tuangalie manufaa ya kiafya tunayopata kutokana na tikitimaji.
1. Huepusha saratani.
Tikitimaji ni moja ya tunda lenye wingi wa kemikali iitwayo ‘’lycopene’’ ambayo pia inapatikana katika matunda mengine pamoja na mboga za majani. Kemikali hii inaaminika kuwa ni kuzuizi na tiba asilia ya saratani ya tezi dume (prostrate cancer) kwa wanaume. Saratani ya aina hii inazidi kushamiri ulimwenguni hivyo ikiwa wewe ni mwanaume wa shoka na hutaki kuwa mmoja wa wagonjwa wa saratani ya aina hii (prostate cancer) ni vyema ukafanya tikitimaji kuwa kimbilio lako.
2. Hupambana na maambukizi mbalimbali yaletayo magonjwa.
Kwa kula tikitimaji unaongeza uwezo wa mwili wako kuwa imara na kujikarabati kwa haraka. Mfano katika ugonjwa wa ngozi, tikitimaji huboresha ngozi yako na kufanya ionekane yenye afya na yenye kunawiri. Hii ni kwasababu tikitimaji lina kemikali iitwayo ‘’amino acid citruline’’ ambayo baadae hubadilisha na kuwa katika mfumo wa kemikali nyingine ‘’arginine’’. Arginine huchochea uzalishwaji wa chembechembe nyeupe za damu ambazo huwa kama kinga katika eneo lenye jeraha. Licha ya hivyo Vitamin C inayopatikana kwenye tikitimaji huongeza kinga ya mwili. Kazi nyingine ya vitamin C ni kuponya vidonda kwakuwa ina uwezo wa kukarabati na kutengeneza sehemu iliyoharibika kwa ugonjwa. Kama wewe una tatizo la vidonda kutopona kwa haraka, tikitimaji pamoja na matunda mengine yenye wingi wa vitamin C ndio chaguo lako.
3. Husafisha figo.
Kwa kuwa asilimia kubwa ya tikitimaji ni maji hivyo maji hayo hufanya tunda hili kuwa ni dawa ya asili inayosaidia figo kuondoa taka mwilini kupitia mkojo. Pia tikitimaji husaidia ini kuvunjavunja na kuondoa sumu mbalimbali na hivyo kurahisisha utendaji mzuri mwili kujisafisha na hatimaye kuwa wenye afya njema.
4. Husaidia kudhibiti ongezeko la shinikizo la damu.(High blood pressure)
Tafiti mbalimbali zilizofanywa na wanasayansi wa chakula dawa, wamebaini kuwa kemikali zinazopatikana katika tikitimaji ‘’L-citrulline’’ ambayo ina uhusiano wa karibu na kemikali nyingine iitwayo ‘’L-arginine’’ zote mbili kwa pamoja zinaaminika kusaidia kupunguza shinikizo la damu (high blood pressure) na hivyo kuepusha maradhi mengine yanayohusiana na moyo.
5. Huongeza hamu na nguvu ya kufanya mapenzi.(Viagra asilia)
Uchunguzi uliofanywa na wataalamu mbalimbali wa afya ukiwemo utafiti kutoka Chuo Kikuu cha Havard Marekani umebaini sio tu kwamba tikitimaji huboresha mfumo wa mzunguko wa damu wa moyo bali hata pia huongeza hamu na nguvu ya kufanya mapenzi kwa wanaume. Kemikali inayojulikana kama ‘’citruline’’ katika tikitimaji inasaidia kuchochea mishipa ya damu ku-relax na kuruhusu damu izunguke kwa ufanisi wake na kuleta muhamko wa uume kama inavyofanya kazi dawa ya kuongeza nguvu ya kufanya mapenzi (Viagra). Tikitimaji pia linaaminika kuongeza nguvu ya mwili kwa asilimia 23%, hii ni kwasababu tikitimaji lina madini ya magnesium ambayo husaidia katika utengenezwaji wa nguvu mwilini (adenosine triphosphate ATP ) na vitamin B6 ambayo huchochea uzalishaji wa hormone ya kukufanya ujisikie mwenye furaha (dopamine hormone).
Angalia hii video clip hapa chini upate maelezo kuhusu tikitimaji kama Viagra asilia kutoka kwenye jarida la afya la Havard University.
Ndugu msomaji, leo tumeona ni jinsi gani tunda hili la tikitimaji lilivyo na faida nyingi katika miili yetu. Ushauri wangu ni kwamba kuliko kunywa soda au kilevu chenye sukari nyingi ni bora kama ukiweza tengeneza juisi yako mwenyewe ya tikitimaji ukiwa nyumbani kwa manufaa ya afya yako na familia yako kiujumla.
NAKUTAKIA AFYA NJEMA!
No comments:
Post a Comment