Saturday, March 15, 2014

Mbinu 12 za kukufanya ushinde na kukubalika kila wakati katika maongezi.

1. Unapoongea na mtu, jitahidi sana msijibizane Inapotokea katika mazungumzo yenu hamjaelewana epuka kurushiana maneno ya hasira. Unachotakiwa kufanya ni kusitisha mazungumzo kwa kumwambia mtaongea wakati mwingine, kwa kufanya hivyo utaepusha ugomvi au jambo lingine baya ambalo lingeweza kutokea. 2. Heshimu mazunguzo yenu, usiwe mkosoaji sana au kujaji kila kitu mwenzako anachosema Kila mtu ana mapungufu yake, lakini wachache sana hupenda kukosolewa nikiwa na maana wengi wetu hatupendi kupingwa kwa yale tunayosema. Tafuta namna nyingine ya kumrekebisha mtu kiuungwana kama anachokisema sio sahihi au ni uongo. 3. Kuwa msikilazaji mzuri kuliko muongeaji sana Namna nzuri ya kuelewa vizuri kile mtu anachosema ni kwa kumsikiliza kwa makini anachokwambia. Anapozungumza mtu unachotakiwa kufanya ni kusikiliza anachokisema na sio kutafakari sana nini cha kumjibu. Muangalie mtu usoni anapoongea na wewe na tikisa kichwa kama unakubaliana nae kuhusu hicho anachokwambia, kwa kumuangalia na kutikisa kichwa kama ishara ya kuonyesha unamuelewa anachokisema humfanya muongeaji ajue kwamba upo nae. 4. Usijaribu kutawala mazungumzo Kama unazungumza na mtu au kundi la watu, jitahidi sana kuwapa nafasi na wengine nao wachangie mawazo yao. Kuongea sana peke yako pasipo kumpa nafasi mtu mwingine naye aongee kutakufanya uonekane mbinafsi na ni mtu mwenye kutaka yako tu yasikilizwe. 5. Changia chochote ulichonacho, mazungumzo huchangamka pale wote mnapoongea na kusikilizana. Sio lazima unapochangia kitu uwe sahihi sana, bali jitahidi kuongelea chochote kinachohusiana na mada mnayozungumzia. Kinachotakiwa katika mazungumzo ni kuonyesha na wewe upo kwa kusema jambo lolote zuri. 6. Jitahidi kulengesha macho yako kwa mtu unayeongea nae Ukimwangalia mtu machoni anapoongea atakuona kwamba unafuatilia anachoongea hivyo utampa moyo wa kuendelea kuzungumza lakini usimkazie macho maana utamfanya asijiamini na kujiona labda anakosea anachokiongea. 7. Tabasamu na onyesha uso wa bashasha kwa mtu/watu unaongea nao Kila mtu hupenda kumwona mwenzake anayeongea ni mwenye furaha. Hata kama una matatizo yako mengine unapokutana na mtu jitahidi kutoonyesha matatizo yako kwake labda kama huyo mtu ni muhimu sana ajue kinachokusibu. 8. Unapozungumza tulia na ongea kwa kujiamini, hii itadhihirisha ni jinsi gani unajua vizuri unachokizungumzia Moja ya sifa ya mwongeaji mzuri ni uwezo wake wa kuongea kwa uhakika na kujiamini kwa kile anachokiwasilisha kwa msikilizaji. Jipange vyema kila unapotaka kuwasilisha jambo kwa watu watakaokusikiliza kuepuka kutoeleweka vizuri kwa wasikilizaji. 9. Kama mtu unayeongea naye ni mgeni kwako, muulize maswali ya kawaida tu pasipo kutaka kujua undani wake Utamshagaza mtu pale utakapomuuliza maswali mengi kwa muda mfupi, watu huchukua muda kuzoeana hivyo ni vyema ukajenga uhusiano imara kwanza kabla ya kutaka kujua mengi kuhusu yeye. Unaweza kuuliza maswali ya kawaida. Mfano:-Unapenda kufanya nini ukiwa nyumbani? -Una familia ya watoto wangapi? 10. Jitahidi kujidhibiti usipayuke au kuzungumza kwa sauti ya chini Ongea kwa sauti ambayo msikilizaji anaweza kukusikia, kama unasisitiza kitu basi ongeza sauti kiasi kwa namna ya kuonyesha msisitizo. 11. Jitahidi kuwa mkweli na ujue nini unaongea kwa mtu anayekusikiliza kwani hakuna mtu unayependa kusikiliza uongo Hata kama ni wewe hutopenda kusikiliza umbea usio wa maana, ni hivyo pia kwa mtu mwingine. Kumbuka kwa kadri mtu anavyokusikia kila siku unazungumza uongo ndivyo anavyopungukiwa imani na wewe. Uaminifu ni kitu cha gharama sana. Chunga usipoteze uaminifu wako kwasababu ya vitu vidogo vidogo kama kusema uongo. 12. Jitahidi kujua mambo mengi kwa kusoma magazeti, kusikiliza redio au kuangalia televisheni kiasi fulani ili upate uwanja mpana wa kuongelea chochote mnachozungumza. Utashangaza watu ikiwa utakosa chochote cha kuongea iwapo utapewa nafasi ya kusema kitu, jifunze mambo mengi kwa kusoma, kusikiliza na kuangalia vyombo vya habari ujue nini wenzako wanafanya ulimwenguni. Sio lazima uwe muongeaji mzuri sana bali ni vyema uwe mtu mwenye mawazo mapana na mambo mazuri ya kuongea na watu kila unapopata nafasi ya kuongea.

No comments:

Post a Comment