Sunday, March 23, 2014

Njia 7 za kudhibiti hasira.

Kila mtu hukasirika pale anapochukizwa au kukasirishwa na jambo fulani, hali hii humtokea mtu yeyote. Ikiwa utaruhusu hasira zikutawale zitakupelekea kuvuruga akili yako na hatimaye kudhoofisha afya yako. Hasira sio kitu kizuri kabisa, hasira inaweza kuwa ni ya kubomoa au kujenga lakini mara nyingi hasira husababisha hasara kwa kuwa inabomoa na kuharibu mambo. Tuangalie hii mifano miwili; *.Unaingia nyumbani na kukuta sebuleni kumekaa hovyo makochi, meza na vitu vingine vimekaa shagara bagara. Unakasirika na kuona vitu vimekaa vibaya na kuamua kupanga na kuweka kila kitu sawa. Baada ya muda sebule inaonekana ni yenye kupendeza tena. *.Mzazi wako anaongea na wewe na kukuomba umueleze kwanini umechelewa kurudi nyumbani. Unakasirika na kuamua kumfokea hadi kutaka kupigana. Baada ya muda mzazi wako anachukizwa kwa kile ulichofanya na wote mnakuwa katika hali mbaya ya kutoelewana.Katika mifano hiyo miwili hapo juu tunaona ni jinsi gani hasira inaweza kukujenga na kukufanya ufanye jambo kwa ari na kwa nguvu zako zote vilevile hasira inaweza kuharibu mambo na kukupelekea uwe katika hali ya majuto. Hizi hapa ni njia 7 za kukusaidia kutuliza hasira zako 1. Fikiri kabla hujaongea Unapojihisi unashindwa kujitawala na kupandisha hasira. Ni vyema ukakaa kimya au kuondoka kabisa mahali ulipo ili kuepusha shari au kuongea mambo ambayo yatakufanya ujute hapo baadae. Utakaponyamaza ni rahisi hata kwa mtu/watu unaongea nao kutulia kwakuwa hutoonyesha dalili ya kutaka kujibizana. Ikiwa mtu atakulazimisha kwa namna moja au nyingine uongee basi ni vyema ukamwambia sipo tayari kuongea na wewe kwa sasa labda baadae na ondoka katika eneo hilo bila kusema neno lingine lolote. 2. Vuta pumzi Unapopandisha hasira, mapigo yako ya moyo yanaongezeka kwa kasi, nguvu nazo zinaongezeka na mwili wako unakuwa tayari kufanya lolote pasipo kufikiri na kushindwa kujitawala. Kufikia hatua hiyo ni hali mbaya sana inayoweza kukupelekea kufanya jambo lolote la hatari. Hali hiyo inapaswa kudhibitiwa na wewe mwenyewe kabla hujakuwa na hasira zaidi. Itakubidi ushushe hasira zako kwa kukaa chini na kutulia kisha vuta pumzi, jitahidi kuhimili mihemko yako ya mwili kwa kutofanya lolote bali kutulia na kuvuta pumzi na kupumua angalau kwa dakika 5. Vuta pumzi ndani taratibu na kwa wingi kisha pumua. Baada ya dakika 2-3 bila shaka utaanza kujisikia mwenye amani. 3. Nenda mahali penye amani au popote penye kuleta furaha Ukiwa na hasira iliyokutawala kwa muda mrefu ni vyema ukaenda mahali ambapo unaweza kupata furaha mfano kwenye fukwe za bahari au ziwa (beach), bustani nzuri yenye majani na maua ya kupendeza au mahali ambapo kuna mkusanyiko wa watu wengi na shughuli za kijamii zinafanyika kama kwenye stadium (uwanja wa mpira wa miguu, kikapu, nyavu n.k) na pengine popote pale ambapo unaweza ukaondoa mawazo mabaya na kujifariji. 4. Hesabu namba kichwani 1 mpaka 20 Unaweza kuona mbinu hii ya kuhesabu namba kama haina maana lakini ikiwa utaitumia itakusaidia kuondoa mawazo ya kitu au mtu aliyekukasirisha na kuweza kujimudu kupambana na hasira zako. Vuta pumzi na kisha pumua taratibu, anza kuhesabu namba kuanzia 1 kupanda mpaka 20 bila kufikiri chochote isipokuwa weka mawazo yako katika kuhesabu namba. Usiruhusu mtu akukatishe hivyo itabidi ukae mahali peke yako au ikiwezekana tulia na hesabu namba zako bila kusikiliza chochote. 5. Eleza shida yako au kitu kinachokukera kwa mtu wako wa karibu unayemuamini Kueleza mambo yanayokusibu kwa mtu mwingine ni njia nzuri ya kutoa kero zako zinazokufanya ukasirike. Mtu wako wa karibu anaweza kuwa mzazi, shangazi, kaka au jamaa yako. Ikiwa utaeleza kero zako kwa mtu wako wa karibu utatoa yaliyo moyoni mwako na kuwa mwenye amani. Pia utakapomueleza mtu yanayokusibu ni rahisi kupata ushauri mzuri kutoka kwake ambao huenda utakusaidia kutatua tatizo lako. 6. Epuka kuwa karibu na mtu au kitu kinachokuchukiza Unaweza kuwa unakasirika kila umuonapo mtu fulani usiyempenda, pia unaweza kuwa unakasirika kila uonapo kitu fulani usichokipenda. Chochote kinachokufanya ukasirike ni vyema ukakiepuka ili usichukie. Kama ni mtu fulani ndiye anakusababisha ukasirike ni vyema ukatafuta ufumbuzi wa mgogoro wenu na kuweka mambo sawa. 7. Fanya zoezi lolote la kuchangamsha mwili Jishughulishe na mchezo wowote au mazoezi kama kuogelea, kuendesha baiskeli, kukimbia angalau kilomita 2 au tembea kwa miguu kwa umbali fulani. Lengo ni kubadilisha mazingira, kufikiri na kuona mengine kuliko kukaa sehemu moja na kufikiri mambo hayo hayo yanayokusabibisha upate hasira.

Saturday, March 15, 2014

Mbinu 12 za kukufanya ushinde na kukubalika kila wakati katika maongezi.

1. Unapoongea na mtu, jitahidi sana msijibizane Inapotokea katika mazungumzo yenu hamjaelewana epuka kurushiana maneno ya hasira. Unachotakiwa kufanya ni kusitisha mazungumzo kwa kumwambia mtaongea wakati mwingine, kwa kufanya hivyo utaepusha ugomvi au jambo lingine baya ambalo lingeweza kutokea. 2. Heshimu mazunguzo yenu, usiwe mkosoaji sana au kujaji kila kitu mwenzako anachosema Kila mtu ana mapungufu yake, lakini wachache sana hupenda kukosolewa nikiwa na maana wengi wetu hatupendi kupingwa kwa yale tunayosema. Tafuta namna nyingine ya kumrekebisha mtu kiuungwana kama anachokisema sio sahihi au ni uongo. 3. Kuwa msikilazaji mzuri kuliko muongeaji sana Namna nzuri ya kuelewa vizuri kile mtu anachosema ni kwa kumsikiliza kwa makini anachokwambia. Anapozungumza mtu unachotakiwa kufanya ni kusikiliza anachokisema na sio kutafakari sana nini cha kumjibu. Muangalie mtu usoni anapoongea na wewe na tikisa kichwa kama unakubaliana nae kuhusu hicho anachokwambia, kwa kumuangalia na kutikisa kichwa kama ishara ya kuonyesha unamuelewa anachokisema humfanya muongeaji ajue kwamba upo nae. 4. Usijaribu kutawala mazungumzo Kama unazungumza na mtu au kundi la watu, jitahidi sana kuwapa nafasi na wengine nao wachangie mawazo yao. Kuongea sana peke yako pasipo kumpa nafasi mtu mwingine naye aongee kutakufanya uonekane mbinafsi na ni mtu mwenye kutaka yako tu yasikilizwe. 5. Changia chochote ulichonacho, mazungumzo huchangamka pale wote mnapoongea na kusikilizana. Sio lazima unapochangia kitu uwe sahihi sana, bali jitahidi kuongelea chochote kinachohusiana na mada mnayozungumzia. Kinachotakiwa katika mazungumzo ni kuonyesha na wewe upo kwa kusema jambo lolote zuri. 6. Jitahidi kulengesha macho yako kwa mtu unayeongea nae Ukimwangalia mtu machoni anapoongea atakuona kwamba unafuatilia anachoongea hivyo utampa moyo wa kuendelea kuzungumza lakini usimkazie macho maana utamfanya asijiamini na kujiona labda anakosea anachokiongea. 7. Tabasamu na onyesha uso wa bashasha kwa mtu/watu unaongea nao Kila mtu hupenda kumwona mwenzake anayeongea ni mwenye furaha. Hata kama una matatizo yako mengine unapokutana na mtu jitahidi kutoonyesha matatizo yako kwake labda kama huyo mtu ni muhimu sana ajue kinachokusibu. 8. Unapozungumza tulia na ongea kwa kujiamini, hii itadhihirisha ni jinsi gani unajua vizuri unachokizungumzia Moja ya sifa ya mwongeaji mzuri ni uwezo wake wa kuongea kwa uhakika na kujiamini kwa kile anachokiwasilisha kwa msikilizaji. Jipange vyema kila unapotaka kuwasilisha jambo kwa watu watakaokusikiliza kuepuka kutoeleweka vizuri kwa wasikilizaji. 9. Kama mtu unayeongea naye ni mgeni kwako, muulize maswali ya kawaida tu pasipo kutaka kujua undani wake Utamshagaza mtu pale utakapomuuliza maswali mengi kwa muda mfupi, watu huchukua muda kuzoeana hivyo ni vyema ukajenga uhusiano imara kwanza kabla ya kutaka kujua mengi kuhusu yeye. Unaweza kuuliza maswali ya kawaida. Mfano:-Unapenda kufanya nini ukiwa nyumbani? -Una familia ya watoto wangapi? 10. Jitahidi kujidhibiti usipayuke au kuzungumza kwa sauti ya chini Ongea kwa sauti ambayo msikilizaji anaweza kukusikia, kama unasisitiza kitu basi ongeza sauti kiasi kwa namna ya kuonyesha msisitizo. 11. Jitahidi kuwa mkweli na ujue nini unaongea kwa mtu anayekusikiliza kwani hakuna mtu unayependa kusikiliza uongo Hata kama ni wewe hutopenda kusikiliza umbea usio wa maana, ni hivyo pia kwa mtu mwingine. Kumbuka kwa kadri mtu anavyokusikia kila siku unazungumza uongo ndivyo anavyopungukiwa imani na wewe. Uaminifu ni kitu cha gharama sana. Chunga usipoteze uaminifu wako kwasababu ya vitu vidogo vidogo kama kusema uongo. 12. Jitahidi kujua mambo mengi kwa kusoma magazeti, kusikiliza redio au kuangalia televisheni kiasi fulani ili upate uwanja mpana wa kuongelea chochote mnachozungumza. Utashangaza watu ikiwa utakosa chochote cha kuongea iwapo utapewa nafasi ya kusema kitu, jifunze mambo mengi kwa kusoma, kusikiliza na kuangalia vyombo vya habari ujue nini wenzako wanafanya ulimwenguni. Sio lazima uwe muongeaji mzuri sana bali ni vyema uwe mtu mwenye mawazo mapana na mambo mazuri ya kuongea na watu kila unapopata nafasi ya kuongea.

Saturday, March 8, 2014

Njia 19 za kukufanya uonekane unajiamini.

Kujiamini kwako kutakufanya uonekane wewe ni mwanaume au mwanamke mwenye uhakika na mahiri katika kazi zako. Licha ya hivyo ikiwa utapendeza kwa kuvaa vizuri yani kuwa maridadi na nadhimu utaonekana unajipenda na mwenye utashi wa kufanya vyema katika shughuli zako au jambo lolote lile. Kila mtu huvutiwa na kujiamini kwa mtu katika mambo yake hivyo ikiwa nawe unataka uonekane unajiamini soma hizi njia 19 zikusaidie kuongeza wasifu wako wa kujiamini. 1. Jijengee mazoea ya kuongea kwa sauti kubwa ya kusikika vizuri na epuka kutamka maneno vibaya. 2. Unapokuwa umesimama simama wima, usiweke mikono mfukoni na pia usijiegemeze kwenye kitu kingine mfano meza, ukuta, nguzo nakadhalika. 3. Unapoongea na mtu jipe nafasi ya kutosha kwa kuwa karibu na mtu unayeongea naye bila kumsogelea sana, yatawale mazingira yako. Tumia mikono yako kuelewesha kile unachokisema. Kama umekaa kwenye kiti basi kaa kistaarabu, pia unaweza weka miguu yako mkao wa kukunja nne lakini chunga usijilegeze na kuonekana umejitandaza. 4. Wakati wote jitahidi kutulia bila kujionyesha una wasiwasi. Ondoa wasiwasi unaoweza kukufanya usikae mahali kwa amani. Tulia bila kuhofia kitu chochote, pumua taratibu na utajisikia vizuri mapigo yako ya moyo yatakuwa sawa na mwili wako utapata nguvu. 5. Unapoongea na mtu muangalie machoni kwa kuonyesha uso wa bashasha. Kuwa makini kumsikiliza na tikisa kichwa pale unapoafiki anachokuambia kama ishara ya kuwa unampata na kuelewa anachokwambia lakini usimkodolee macho sana. Unaweza pepesa macho pembeni lakini isiwe mara nyingi sana kuonekana husikilizi au una aibu. 6. Jiheshimu na jithamini uwe mtu wa kuheshimiwa. Watu watakuchukulia kwa namna utakavyojiweka. Kwa kadri utakavyojiheshimu na kujiona wewe yu jasiri ndivyo watu pia watakavyokuona. 7. Unapotaka kuangalia pembeni, zungusha kichwa upande kuelekea mahali unapotaka kutazama bila kujigeuza mwili mzima. Tazama bila kupepesa macho sana kuonekana unahofia kitu fulani. 8. Jitahidi sana kuwa mwenyewe, usitake kuigiza mtu mwingine anachofanya. Unaweza kujifanya kama mtu fulani kwa muda ikiwa tu unataka kujifunza kujiamini na kuwa kama yeye. Lakini utakapokuwa umeshajenga ujasiri ni vizuri ujiongoze mwenyewe kwa kufanya mazoezi zaidi ya kuongeza ujasiri wako. (Mfano kwa kuongea mbele ya umati wa watu, kujieleza na kumshawishi mtu afanye unalotaka nk) 9. Kama unategemea kuwasilisha ujumbe kwenye mhadhara au mkutano (kwa maana ya kufanya presentation) jiandae vyema na mapema kabisa hasa pale presentation inapokuhitaji uwe na notes au muongozo wa nini unatakiwa uwasilishe ili kuepusha kutoweza kusoma na kutamka baadhi ya maneno vizuri. 10. Vuta pumzi kila unapokuwa na hofu ya kushindwa kufanya kitu fulani kisha jiambie "NAWEZA" kisha fanya kitu hicho bila kufikiria kuwa utashindwa. 11. Fanya mambo yako kwa umakini na jiamini kuwa kila kitu kitakwenda vizuri, kwa kufanya hivyo utaonekana kwa watu unajiamini kwa kile unachoweza kufanya. Ni vizuri kujenga hisia za ujasiri ndani yako kuwa UNAWEZA kufanya lolote bila uwoga. 13. Unapokuwa unaongea na kuhisi sauti yako haitoki vizuri, kunywa maji kama unadhani mate yatakuwa yamekukauka na rekebisha koo kisha hesabu 1, 2, 3 mpaka 20 kwa kupaza sauti kwa kadri unavyokaribia kufika ishirini. 14. Unapoongea na mtu/watu zaidi ya wawili, jitahidi kumiliki ujumbe wako kwa kueleza vizuri kile unachosema. Kama hutoweza kusema vizuri ni rahisi mtu mwingine kukusaidia kuelezea hivyo utaonekeana hujajipanga. Jipange vizuri kwa kujua nini unataka kuongea kabla ya kuanza kuzungumza. 15. Ongea kwa kutamka maneno vizuri bila kwenda mbio na jitahidi kutoongea sana. Ongea kwa kiasi kisha tulia kwa sekunde kisha endelea. Hakuna sababu ya kutaka kuongea mengi bila kusimama lengo ni ujumbe ufike kwa wale wanaokusikiliza. Ukiongea kwa haraka utaonekana hufahamu vizuri unachokisema hivyo unataka kumaliza haraka. 16. Onyesha kujipenda kwa kutabasamu au kucheka kila unapofurahishwa na jambo fulani. Amini usiamini tabasamu humfanya mtu aonekane hana wasiwasi wowote kwa kuwa anajiamini. 17. Unapoongea unaweza pia kutumia misemo iliyowahi kusemwa na watu wengine kuhusiana na mada mnayoongelea ili kuongeza msisitizo wa kile mnachokiongelea. 18. Unaposhindwa na jambo jitahidi kutokuonyesha umejisikia vibaya kushindwa. Kukunja sura kwa huzuni au kwa kukasirika baada ya kushindwa jambo fulani kutakufanya uonekane umefadhaishwa na aibu. 19. Ni muhimu kuonyesha uaminifu na uadilifu wako kwa watu. Kujiamini kunaendana na kuaminika. Ukiwa unajiamini halafu huna maana kwa watu ni sawa na kujigamba pasipo kuwa na lolote la kujivunia. Jisikie kuwa wewe ni jasiri na mwingi wa furaha, onyesha uungwana wako kwa watu nao watakuthamini. Kama unachochote cha kuongeza kuhusiana na mada hapo juu, tafadhali usisite kutoa maoni yako!