Tuesday, April 15, 2014

Ongeza furaha yako kwa kujipenda.

Unayo kila sababu ya kufanya wiki yako kuwa ya kipekee kwa kupanga mambo yako kwenda vizuri kama utakavyo. Itapendeza kama kila siku ya wiki utafanya kazi zako katika mpangilio unaoeleweka na kukamilisha kazi zote kikamilifu kama ulivyokusudia. Siku za wiki huisha haraka sana, kama hutokuwa umejipanga vyema utajikuta wakati umepita ukiwa bado hujafanya lolote hivyo ni muhimu sana upange wiki yako vizuri na mapema kabla ya kuanza juma lingine upya. Wengi wetu tumezoea kupitisha siku kawaida tu kwa maana ya hatufanyi mabadiliko yoyote kati ya jana na leo. Itakuwa ni busara kama kila siku yako ikiwa ni tofauti na nyingine. Ni vyema ukafanya tathmini ya kazi zako zote ulizopanga kufanya wiki iliyopita na ujiulize je umeweza kukamilisha ipasavyo? Ikiwa utaona mambo hayakwenda vizuri ni vyema ukafanya mabadiliko. Mabadiliko yenyewe yataanza kwa kujiuliza kwanini mambo yako hayajakwenda sawa? Majibu utakayopata yatafakari kwa makini yakusaidie kukuongoza na kukurekebisha. Tabia nzuri zitakazokufanya ufanikishe hayo ni kama kuachana na uvivu na kuwa mtekelezaji wa kazi zako, jifunze kutumia muda wako vizuri, kuwa na mazoea ya kujifunza mambo mbalimbali yatakayokusaidia hapo baadae. Hizi hapa ni njia 6 za kupanga wiki yako leo zikusaidie kufanya yale yote upendayo 1. Andika chini kwenye karatasi chochote ambacho ni muhimu kwako Unapenda nini? Unaamini nini kinachokufanya ufurahie maisha yako na kukupa motisha ya kufanya kazi zako kwa moyo mmoja wa furaha. Ukijua nini unapenda na kufanyia kazi upendacho utaongeza utashi wako na hatimaye utafahamu maana halisi ya maisha yako. Kujitambua ndio mwanzo wa kujua vipawa vyako. 2. Jiwekee ratiba maalum kila jumapili kuwa ni siku ya kupanga yale yote unayotaka kufanya wiki ijayo Itategemea na kazi yako ilivyo, muhimu ni kuwa na mpangilio mzuri wa kazi zako kwa namna yeyote ile unavyoona inafaa. Kujipanga ni bora kuliko kutofanya lolote kabisa. Jiwekee mipango ya shughuli zako za wiki kwa kujua nini utafanya kuanzia siku ya jumatatu hadi jumamosi. Andika kwenye kitabu chako cha kazi chochote unachohitaji kukamilisha iwe ni shughuli ndogo au kubwa muhimu ni kujua je kazi yenyewe inatekelekeza? Kama jibu ni NDIYO weka kazi hiyo kwenye orodha ya kazi unazokusudia kukamilisha ndani muda fulani kulingana na ratiba yako ya wiki. 3. Jijengee mazoea ya kuangalia kalenda ya kazi zako, jua ni matukio gani yanafuata wiki ijayo ili ujiandae vizuri Angalia tarehe muhimu za matukio yajayo kama kuna mkutano wowote, una appointment na mtu au shughuli maalum inayokaribia kufanyika ili ujipange na kujiandaa mapema. Kumbuka ukiwa na mpango mzuri hakuna kitu kitakachoharibika kwakuwa utakuwa umejiandaa kwa lolote litakalojitokeza kuingilia mipango yako. 4. Panga kazi zako kwa mpangilio mzuri na rahisi kwako kuweza kutekeleza Usipange mambo mengi yafanyike ndani ya muda mfupi, utachanganya mambo na kushindwa kutekeleza yote. Jua kipi kianze na kipi kitafuata na utekeleze kila jambo kwa wakati wake. Do First Things First usirundike kazi nyingi katika siku moja. Fanya kila kazi kulingana na uzito wake na muda stahiki unaohitajika kufanya kazi hiyo. Jipe nafasi kwa kufanya kazi zako kwa ufanisi na muda wa kutosha. 5. Panga muda maalum wa kupumzika na wakufanya kazi zako. Hii itakusaidia kufanya kazi bila kujichosha na kuwa mwenye furaha kazini Fanya shughuli zako kwa bidii lakini usijifanyishe kazi kipita kiasi. Pima uzito wa kazi ujue utaifanya kwa muda gani na utilie uzito kiasi gani. Tumia nguvu na muda stahiki kufanya kazi husika kwa maana ya usitumie muda mwingi na nguvu nyingi kufanya kazi inayohitaji muda mfupi kukamilika. Hii imekaa vizuri kwa wale waliojiajiri lakini pia hata kama umeajiriwa jitahidi kufanya kazi kwa kadri unavyoweza bila kusahau kupumzika. 6. Kila mwisho wa siku fanya tathmini ya mafanikio ya malengo yako Huwezi jua umefanya nini cha maana ikiwa hujajiwekea malengo. Ukiwa na malengo ni rahisi kujua umepiga hatua kimaendeleo kwa kiasi gani. Ni muhimu kuweka kumbukumbu ya kila mafanikio unayopata ili kujua wapi umefanya vizuri na wapi kazi imedorora.