Sunday, March 23, 2014

Njia 7 za kudhibiti hasira.

Kila mtu hukasirika pale anapochukizwa au kukasirishwa na jambo fulani, hali hii humtokea mtu yeyote. Ikiwa utaruhusu hasira zikutawale zitakupelekea kuvuruga akili yako na hatimaye kudhoofisha afya yako. Hasira sio kitu kizuri kabisa, hasira inaweza kuwa ni ya kubomoa au kujenga lakini mara nyingi hasira husababisha hasara kwa kuwa inabomoa na kuharibu mambo. Tuangalie hii mifano miwili; *.Unaingia nyumbani na kukuta sebuleni kumekaa hovyo makochi, meza na vitu vingine vimekaa shagara bagara. Unakasirika na kuona vitu vimekaa vibaya na kuamua kupanga na kuweka kila kitu sawa. Baada ya muda sebule inaonekana ni yenye kupendeza tena. *.Mzazi wako anaongea na wewe na kukuomba umueleze kwanini umechelewa kurudi nyumbani. Unakasirika na kuamua kumfokea hadi kutaka kupigana. Baada ya muda mzazi wako anachukizwa kwa kile ulichofanya na wote mnakuwa katika hali mbaya ya kutoelewana.Katika mifano hiyo miwili hapo juu tunaona ni jinsi gani hasira inaweza kukujenga na kukufanya ufanye jambo kwa ari na kwa nguvu zako zote vilevile hasira inaweza kuharibu mambo na kukupelekea uwe katika hali ya majuto. Hizi hapa ni njia 7 za kukusaidia kutuliza hasira zako 1. Fikiri kabla hujaongea Unapojihisi unashindwa kujitawala na kupandisha hasira. Ni vyema ukakaa kimya au kuondoka kabisa mahali ulipo ili kuepusha shari au kuongea mambo ambayo yatakufanya ujute hapo baadae. Utakaponyamaza ni rahisi hata kwa mtu/watu unaongea nao kutulia kwakuwa hutoonyesha dalili ya kutaka kujibizana. Ikiwa mtu atakulazimisha kwa namna moja au nyingine uongee basi ni vyema ukamwambia sipo tayari kuongea na wewe kwa sasa labda baadae na ondoka katika eneo hilo bila kusema neno lingine lolote. 2. Vuta pumzi Unapopandisha hasira, mapigo yako ya moyo yanaongezeka kwa kasi, nguvu nazo zinaongezeka na mwili wako unakuwa tayari kufanya lolote pasipo kufikiri na kushindwa kujitawala. Kufikia hatua hiyo ni hali mbaya sana inayoweza kukupelekea kufanya jambo lolote la hatari. Hali hiyo inapaswa kudhibitiwa na wewe mwenyewe kabla hujakuwa na hasira zaidi. Itakubidi ushushe hasira zako kwa kukaa chini na kutulia kisha vuta pumzi, jitahidi kuhimili mihemko yako ya mwili kwa kutofanya lolote bali kutulia na kuvuta pumzi na kupumua angalau kwa dakika 5. Vuta pumzi ndani taratibu na kwa wingi kisha pumua. Baada ya dakika 2-3 bila shaka utaanza kujisikia mwenye amani. 3. Nenda mahali penye amani au popote penye kuleta furaha Ukiwa na hasira iliyokutawala kwa muda mrefu ni vyema ukaenda mahali ambapo unaweza kupata furaha mfano kwenye fukwe za bahari au ziwa (beach), bustani nzuri yenye majani na maua ya kupendeza au mahali ambapo kuna mkusanyiko wa watu wengi na shughuli za kijamii zinafanyika kama kwenye stadium (uwanja wa mpira wa miguu, kikapu, nyavu n.k) na pengine popote pale ambapo unaweza ukaondoa mawazo mabaya na kujifariji. 4. Hesabu namba kichwani 1 mpaka 20 Unaweza kuona mbinu hii ya kuhesabu namba kama haina maana lakini ikiwa utaitumia itakusaidia kuondoa mawazo ya kitu au mtu aliyekukasirisha na kuweza kujimudu kupambana na hasira zako. Vuta pumzi na kisha pumua taratibu, anza kuhesabu namba kuanzia 1 kupanda mpaka 20 bila kufikiri chochote isipokuwa weka mawazo yako katika kuhesabu namba. Usiruhusu mtu akukatishe hivyo itabidi ukae mahali peke yako au ikiwezekana tulia na hesabu namba zako bila kusikiliza chochote. 5. Eleza shida yako au kitu kinachokukera kwa mtu wako wa karibu unayemuamini Kueleza mambo yanayokusibu kwa mtu mwingine ni njia nzuri ya kutoa kero zako zinazokufanya ukasirike. Mtu wako wa karibu anaweza kuwa mzazi, shangazi, kaka au jamaa yako. Ikiwa utaeleza kero zako kwa mtu wako wa karibu utatoa yaliyo moyoni mwako na kuwa mwenye amani. Pia utakapomueleza mtu yanayokusibu ni rahisi kupata ushauri mzuri kutoka kwake ambao huenda utakusaidia kutatua tatizo lako. 6. Epuka kuwa karibu na mtu au kitu kinachokuchukiza Unaweza kuwa unakasirika kila umuonapo mtu fulani usiyempenda, pia unaweza kuwa unakasirika kila uonapo kitu fulani usichokipenda. Chochote kinachokufanya ukasirike ni vyema ukakiepuka ili usichukie. Kama ni mtu fulani ndiye anakusababisha ukasirike ni vyema ukatafuta ufumbuzi wa mgogoro wenu na kuweka mambo sawa. 7. Fanya zoezi lolote la kuchangamsha mwili Jishughulishe na mchezo wowote au mazoezi kama kuogelea, kuendesha baiskeli, kukimbia angalau kilomita 2 au tembea kwa miguu kwa umbali fulani. Lengo ni kubadilisha mazingira, kufikiri na kuona mengine kuliko kukaa sehemu moja na kufikiri mambo hayo hayo yanayokusabibisha upate hasira.

Saturday, March 15, 2014

Mbinu 12 za kukufanya ushinde na kukubalika kila wakati katika maongezi.

1. Unapoongea na mtu, jitahidi sana msijibizane Inapotokea katika mazungumzo yenu hamjaelewana epuka kurushiana maneno ya hasira. Unachotakiwa kufanya ni kusitisha mazungumzo kwa kumwambia mtaongea wakati mwingine, kwa kufanya hivyo utaepusha ugomvi au jambo lingine baya ambalo lingeweza kutokea. 2. Heshimu mazunguzo yenu, usiwe mkosoaji sana au kujaji kila kitu mwenzako anachosema Kila mtu ana mapungufu yake, lakini wachache sana hupenda kukosolewa nikiwa na maana wengi wetu hatupendi kupingwa kwa yale tunayosema. Tafuta namna nyingine ya kumrekebisha mtu kiuungwana kama anachokisema sio sahihi au ni uongo. 3. Kuwa msikilazaji mzuri kuliko muongeaji sana Namna nzuri ya kuelewa vizuri kile mtu anachosema ni kwa kumsikiliza kwa makini anachokwambia. Anapozungumza mtu unachotakiwa kufanya ni kusikiliza anachokisema na sio kutafakari sana nini cha kumjibu. Muangalie mtu usoni anapoongea na wewe na tikisa kichwa kama unakubaliana nae kuhusu hicho anachokwambia, kwa kumuangalia na kutikisa kichwa kama ishara ya kuonyesha unamuelewa anachokisema humfanya muongeaji ajue kwamba upo nae. 4. Usijaribu kutawala mazungumzo Kama unazungumza na mtu au kundi la watu, jitahidi sana kuwapa nafasi na wengine nao wachangie mawazo yao. Kuongea sana peke yako pasipo kumpa nafasi mtu mwingine naye aongee kutakufanya uonekane mbinafsi na ni mtu mwenye kutaka yako tu yasikilizwe. 5. Changia chochote ulichonacho, mazungumzo huchangamka pale wote mnapoongea na kusikilizana. Sio lazima unapochangia kitu uwe sahihi sana, bali jitahidi kuongelea chochote kinachohusiana na mada mnayozungumzia. Kinachotakiwa katika mazungumzo ni kuonyesha na wewe upo kwa kusema jambo lolote zuri. 6. Jitahidi kulengesha macho yako kwa mtu unayeongea nae Ukimwangalia mtu machoni anapoongea atakuona kwamba unafuatilia anachoongea hivyo utampa moyo wa kuendelea kuzungumza lakini usimkazie macho maana utamfanya asijiamini na kujiona labda anakosea anachokiongea. 7. Tabasamu na onyesha uso wa bashasha kwa mtu/watu unaongea nao Kila mtu hupenda kumwona mwenzake anayeongea ni mwenye furaha. Hata kama una matatizo yako mengine unapokutana na mtu jitahidi kutoonyesha matatizo yako kwake labda kama huyo mtu ni muhimu sana ajue kinachokusibu. 8. Unapozungumza tulia na ongea kwa kujiamini, hii itadhihirisha ni jinsi gani unajua vizuri unachokizungumzia Moja ya sifa ya mwongeaji mzuri ni uwezo wake wa kuongea kwa uhakika na kujiamini kwa kile anachokiwasilisha kwa msikilizaji. Jipange vyema kila unapotaka kuwasilisha jambo kwa watu watakaokusikiliza kuepuka kutoeleweka vizuri kwa wasikilizaji. 9. Kama mtu unayeongea naye ni mgeni kwako, muulize maswali ya kawaida tu pasipo kutaka kujua undani wake Utamshagaza mtu pale utakapomuuliza maswali mengi kwa muda mfupi, watu huchukua muda kuzoeana hivyo ni vyema ukajenga uhusiano imara kwanza kabla ya kutaka kujua mengi kuhusu yeye. Unaweza kuuliza maswali ya kawaida. Mfano:-Unapenda kufanya nini ukiwa nyumbani? -Una familia ya watoto wangapi? 10. Jitahidi kujidhibiti usipayuke au kuzungumza kwa sauti ya chini Ongea kwa sauti ambayo msikilizaji anaweza kukusikia, kama unasisitiza kitu basi ongeza sauti kiasi kwa namna ya kuonyesha msisitizo. 11. Jitahidi kuwa mkweli na ujue nini unaongea kwa mtu anayekusikiliza kwani hakuna mtu unayependa kusikiliza uongo Hata kama ni wewe hutopenda kusikiliza umbea usio wa maana, ni hivyo pia kwa mtu mwingine. Kumbuka kwa kadri mtu anavyokusikia kila siku unazungumza uongo ndivyo anavyopungukiwa imani na wewe. Uaminifu ni kitu cha gharama sana. Chunga usipoteze uaminifu wako kwasababu ya vitu vidogo vidogo kama kusema uongo. 12. Jitahidi kujua mambo mengi kwa kusoma magazeti, kusikiliza redio au kuangalia televisheni kiasi fulani ili upate uwanja mpana wa kuongelea chochote mnachozungumza. Utashangaza watu ikiwa utakosa chochote cha kuongea iwapo utapewa nafasi ya kusema kitu, jifunze mambo mengi kwa kusoma, kusikiliza na kuangalia vyombo vya habari ujue nini wenzako wanafanya ulimwenguni. Sio lazima uwe muongeaji mzuri sana bali ni vyema uwe mtu mwenye mawazo mapana na mambo mazuri ya kuongea na watu kila unapopata nafasi ya kuongea.

Saturday, March 8, 2014

Njia 19 za kukufanya uonekane unajiamini.

Kujiamini kwako kutakufanya uonekane wewe ni mwanaume au mwanamke mwenye uhakika na mahiri katika kazi zako. Licha ya hivyo ikiwa utapendeza kwa kuvaa vizuri yani kuwa maridadi na nadhimu utaonekana unajipenda na mwenye utashi wa kufanya vyema katika shughuli zako au jambo lolote lile. Kila mtu huvutiwa na kujiamini kwa mtu katika mambo yake hivyo ikiwa nawe unataka uonekane unajiamini soma hizi njia 19 zikusaidie kuongeza wasifu wako wa kujiamini. 1. Jijengee mazoea ya kuongea kwa sauti kubwa ya kusikika vizuri na epuka kutamka maneno vibaya. 2. Unapokuwa umesimama simama wima, usiweke mikono mfukoni na pia usijiegemeze kwenye kitu kingine mfano meza, ukuta, nguzo nakadhalika. 3. Unapoongea na mtu jipe nafasi ya kutosha kwa kuwa karibu na mtu unayeongea naye bila kumsogelea sana, yatawale mazingira yako. Tumia mikono yako kuelewesha kile unachokisema. Kama umekaa kwenye kiti basi kaa kistaarabu, pia unaweza weka miguu yako mkao wa kukunja nne lakini chunga usijilegeze na kuonekana umejitandaza. 4. Wakati wote jitahidi kutulia bila kujionyesha una wasiwasi. Ondoa wasiwasi unaoweza kukufanya usikae mahali kwa amani. Tulia bila kuhofia kitu chochote, pumua taratibu na utajisikia vizuri mapigo yako ya moyo yatakuwa sawa na mwili wako utapata nguvu. 5. Unapoongea na mtu muangalie machoni kwa kuonyesha uso wa bashasha. Kuwa makini kumsikiliza na tikisa kichwa pale unapoafiki anachokuambia kama ishara ya kuwa unampata na kuelewa anachokwambia lakini usimkodolee macho sana. Unaweza pepesa macho pembeni lakini isiwe mara nyingi sana kuonekana husikilizi au una aibu. 6. Jiheshimu na jithamini uwe mtu wa kuheshimiwa. Watu watakuchukulia kwa namna utakavyojiweka. Kwa kadri utakavyojiheshimu na kujiona wewe yu jasiri ndivyo watu pia watakavyokuona. 7. Unapotaka kuangalia pembeni, zungusha kichwa upande kuelekea mahali unapotaka kutazama bila kujigeuza mwili mzima. Tazama bila kupepesa macho sana kuonekana unahofia kitu fulani. 8. Jitahidi sana kuwa mwenyewe, usitake kuigiza mtu mwingine anachofanya. Unaweza kujifanya kama mtu fulani kwa muda ikiwa tu unataka kujifunza kujiamini na kuwa kama yeye. Lakini utakapokuwa umeshajenga ujasiri ni vizuri ujiongoze mwenyewe kwa kufanya mazoezi zaidi ya kuongeza ujasiri wako. (Mfano kwa kuongea mbele ya umati wa watu, kujieleza na kumshawishi mtu afanye unalotaka nk) 9. Kama unategemea kuwasilisha ujumbe kwenye mhadhara au mkutano (kwa maana ya kufanya presentation) jiandae vyema na mapema kabisa hasa pale presentation inapokuhitaji uwe na notes au muongozo wa nini unatakiwa uwasilishe ili kuepusha kutoweza kusoma na kutamka baadhi ya maneno vizuri. 10. Vuta pumzi kila unapokuwa na hofu ya kushindwa kufanya kitu fulani kisha jiambie "NAWEZA" kisha fanya kitu hicho bila kufikiria kuwa utashindwa. 11. Fanya mambo yako kwa umakini na jiamini kuwa kila kitu kitakwenda vizuri, kwa kufanya hivyo utaonekana kwa watu unajiamini kwa kile unachoweza kufanya. Ni vizuri kujenga hisia za ujasiri ndani yako kuwa UNAWEZA kufanya lolote bila uwoga. 13. Unapokuwa unaongea na kuhisi sauti yako haitoki vizuri, kunywa maji kama unadhani mate yatakuwa yamekukauka na rekebisha koo kisha hesabu 1, 2, 3 mpaka 20 kwa kupaza sauti kwa kadri unavyokaribia kufika ishirini. 14. Unapoongea na mtu/watu zaidi ya wawili, jitahidi kumiliki ujumbe wako kwa kueleza vizuri kile unachosema. Kama hutoweza kusema vizuri ni rahisi mtu mwingine kukusaidia kuelezea hivyo utaonekeana hujajipanga. Jipange vizuri kwa kujua nini unataka kuongea kabla ya kuanza kuzungumza. 15. Ongea kwa kutamka maneno vizuri bila kwenda mbio na jitahidi kutoongea sana. Ongea kwa kiasi kisha tulia kwa sekunde kisha endelea. Hakuna sababu ya kutaka kuongea mengi bila kusimama lengo ni ujumbe ufike kwa wale wanaokusikiliza. Ukiongea kwa haraka utaonekana hufahamu vizuri unachokisema hivyo unataka kumaliza haraka. 16. Onyesha kujipenda kwa kutabasamu au kucheka kila unapofurahishwa na jambo fulani. Amini usiamini tabasamu humfanya mtu aonekane hana wasiwasi wowote kwa kuwa anajiamini. 17. Unapoongea unaweza pia kutumia misemo iliyowahi kusemwa na watu wengine kuhusiana na mada mnayoongelea ili kuongeza msisitizo wa kile mnachokiongelea. 18. Unaposhindwa na jambo jitahidi kutokuonyesha umejisikia vibaya kushindwa. Kukunja sura kwa huzuni au kwa kukasirika baada ya kushindwa jambo fulani kutakufanya uonekane umefadhaishwa na aibu. 19. Ni muhimu kuonyesha uaminifu na uadilifu wako kwa watu. Kujiamini kunaendana na kuaminika. Ukiwa unajiamini halafu huna maana kwa watu ni sawa na kujigamba pasipo kuwa na lolote la kujivunia. Jisikie kuwa wewe ni jasiri na mwingi wa furaha, onyesha uungwana wako kwa watu nao watakuthamini. Kama unachochote cha kuongeza kuhusiana na mada hapo juu, tafadhali usisite kutoa maoni yako!

Friday, February 28, 2014

NEW>>UFAFANUZI KUHUSU MATOKEO YA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE (CSEE) 2013.

BARAZA LA MITIHANI LA TANZANIA UFAFANUZI WA MASWALI MBALIMBALI YA WADAU WA ELIMU KUHUSU MATOKEO YA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE (CSEE) 2013 Imetolewa Na: KAIMU KATIBU MTENDAJI 25Februari, 2014 UFAFANUZIWA MASWALI MBALIMBALI YA WADAU WA ELIMUKUHUSU MATOKEO YAMTIHANI WAKIDATO CHA NNE(CSEE)2013 Baraza la Mitihani la Tanzania lilitangaza matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE) 2013 tarehe21/02/2014. Baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Baraza limekuwa likipokea maswali mbalimbali yanayoashiria kuwa baadhi ya wadau wa elimu hawakuelewa vizuri kuhusuViwango vya Ufaulu(grade ranges),alama yachiniya ufaulu(pass mark) naUfaulu wajumlawa mtahiniwa(overall performance). Baraza la Mitihani linapenda kutoa ufafanuzi katika mambo hayo kama ifuatavyo: 1. Viwango vya ufaulu (grade ranges) ni makundi ya alama yanayopangwa ili kuwaweka pamoja watahiniwa wenye uwezo unaofanana katika somo husika na kuwatofautisha na watahiniwa waliopo katika kundi jingine. Makundi haya hupangwa ili kuwawezesha wadau kutambua namna watahiniwa walivyotawanyika katika viwango mbalimbali vya umahiri wa somo husika. Baraza la Mitihani la Tanzania, limekuwa likitumia makundi Matano (5) kwa kipindi kirefu hadi mwaka 2012. Aidha, Kuanzia Mtihani wa Kidato cha Nne(CSEE)2013, Baraza limeanza kutumia utaratibu waMakundi Saba (7)ambayo niA, B+, B, C, D, EnaF. Utaratibu huu umelenga kupunguza mlundikano mkubwa wa alama katika kundi moja. Mgawanyo wa makundi hayo ni kama inavyoonekana kwenye Jedwali la 1. Jedwali Na 1:Viwango vya ufaulu vilivyotumikakatika Matokeo ya CSEE 2013. Kundi Gredi Alama Idadi ya Pointi 1 A 75 - 100 1 2 B+ 60 - 74 2 3 B 50 - 59 3 4 C 40 - 49 4 5 D 30 - 39 5 6 E 20 - 29 6 7 F 0 - 19 7 Aidha, Idadi ya makundi ya ufaulu hutofautiana kati ya nchi na nchi kulingana na mahitaji ya nchi husika. Kwa mfano; Kenya wana makundi Kumi na mbili (12), Malawi Tisa (9), Uganda Tisa (9), Nchi za Afrika magharibi (Nigeria, Ghana, Siera Leone na Liberia) makundi Tisa. 1. Kwa kuzingatia viwango vya ufaulu vilivyoainishwa katika makundi saba yaliyopo kwenye Jedwali na 1, kiwango cha chini cha ufaulu ni gredi D na kiwango cha juu cha ufaulu ni Gredi A. Mtahiniwa atakuwa amefaulu somo husika iwapo atapata gredi D na kuendelea. Aidha, mtahiniwa aliyepata gredi E na F atakuwa hajafaulu somo husika. 1. Madaraja ya ufaulu yamepangwa kwa mujibu wa kifungu cha 20 (1)-(6) cha Kanuni za Mitihani kinachoelekeza kuwa Ufaulu katika daraja la Kwanza hadi la Tatu upangwe kwa kuzingatia jumla ya alama (Points) na Ufaulu katikaDaraja la Nne unapangwa kwa kuzingatia ufaulu wa chini aliopata mtahiniwa ambao ni gredi D katika masomo yasiyopungua mawili au ufaulu kwa kiwango kisichokuwa chini ya Gredi C katika somo moja. Hivyo, madaraja yaliyotumika ni kama yanavyoonekana kwenye Jedwali la 2. Jedwali 2: Madaraja yaliyotumika katika CSEE 2013 Daraja Pointi I 7 - 17 II 18 - 24 III 25 - 31 IV 1. Ufaulu katika somo moja kwa kiwango kisichokuwa chini ya Gredi C au 2. Ufaulu katika masomo yasiyopungua mawili katika Gredi D 0 Alama chini ya D mbili 1. Kwa mujibu wa Kanuni za Mitihani, ufaulu wa somo katika Gredi A hadi C utakuwa ni ufaulu wa “Credit” na Gredi D itahesabika kuwa ni “pass”. Aidha Gredi E na F zitakuwa alama za kufeli. 1. Baraza la mitihani la Tanzania linapenda kutoa taarifa kwamba ufafanuzi wa sifa za kujiunga na mafunzo katika ngazi mbalimbali kwa kutumia mfumo huu mpya wa madaraja utatolewa na mamlaka husika ambapo Kamishna wa Elimu atalitolea ufafanuzi zaidi. Imetolewa Na: KAIMU KATIBU MTENDAJI

Monday, February 10, 2014

Faida nne (4) za kufanya mazoezi ya kukimbia.

Wakati tatizo la unene likiongezeka kwa kasi katika jamii yetu, watu bado wamekuwa wakijisahau kufanyisha mazoezi miili yao licha ya kupata ushauri wa afya katika vyombo vya habari (redioni, T.V, magazetini) na sehemu nyingine mbalimbali wanapotoa huduma za afya. Elimu ya lishe bora pamoja na ile ya kuishi vizuri kwa afya bora ni elimu muhimu sana kwa kila mtu kufahamu. Ukiwa na maarifa ya namna ya kula vizuri na kufanya mazoezi kwa afya, bila shaka utakuwa na upeo mkubwa wa kujua na kuelewa ni jinsi gani chakula na mazoezi yalivyomuhimu kwa maendeleo mazuri ya mwili wako na afya kiujumla. Kuna sababu nyingi za mtu kutofanya mazoezi inaweza kuwa ni maradhi aliyonayo, kutoweka kipaumbele kufanya mazoezi ya mwili, ukosefu wa maarifa nakadhalika lakini swali muhimu la kujiuliza wewe mwenyewe hapa ni, je unasababu yeyote ya msingi ya wewe kutofanya mazoezi? Sababu nzuri ya wewe kutofanya mazoezi inaweza kuwa ni huna muda lakini ni jambo la busara kufikiri je ni kweli unakosa angalau dakika 30 kwa siku kukimbia na kupata muda mwingi wa kutosha wa kulimbikiza mafuta mwilini yanayochangia uzito na unene wa mwili? Zoezi la kukimbia lina manufaa mengi, hizi hapa ni baadhi ya faida. 1. Hurefusha maisha. Uchunguzi wa kisayansi umethibitisha kuwa kukimbia angalau kwa saa chache kwa wiki sio tu kutakufanya uwe mchangamfu na kuongeza utendaji wako wa kazi bali pia huongeza miaka ya kuishi. 2. Huimarisha moyo na mapafu. Kwa mtu wa kawaida mwili hutumia oxygen mara 10 zaidi wakati wa kufanya zoezi rahisi la kukimbia ukilinganisha na akiwa amekaa. Mtu anapofanya zoezi la kupasha mwili kwa muda huimarisha mfumo wa moyo wa usukumaji damu hivyo moyo na mapafu pia hufanya kazi zake kwa ufanisi. 3. Huboresha utendaji kazi wa ubongo na kuongeza uwezo wako wa kufikiri. Ikiwa inaaminika mazoezi ni afya, licha ya kuwa mazoezi yana manufaa mengi kiafya pia inaaminika mazoezi ya kukimbia husababisha ubongo kuzalisha homorne iitwayo ‘’endorphin’’ ambayo kemikali hii huibua hisia za furaha na kumfanya mtu awe katika hali ya kuwa na raha na mwenye mawazo chanya. Sio tu kwamba mazoezi haya yatakufanya ujihisi katika hali ya furaha kwa muda bali yatakufanya pia uongeze ujasiri wako wa kujiamini na kujikubali mwenyewe hivyo pia utapunguza msongo wa mawazo na matatizo mengine yanayosababishwa na kuchoka kwa ubongo. 4. Hupunguza uzito wa mwili na mafuta mwilini. Sote tunajua unapofanya mazoezi, baada ya muda utajisikia kuchoka, kutokwa na jasho, kuhema sana nakadhalika. Haya yote ni matokeo baada ya kufanya zoezi la kukimbia, unapofanya maozezi unachoma calories mwilini na hatimaye kupunguza mafuta. Ikiwa utakuwa unafanya mazoezi ya kukimbia ipasavyo na kwa malengo ni rahisi kwako kuona mabadiliko ya mwili wako baada ya wiki chache. Kama wewe ni mnene na una uzito mkubwa wa mwili huu ndio wakati wako wa kuanza kufanya mazoezi ya kukimbia. Kujua zaidi:Soma Njia za kupunguza unene wa mwili wako. Kumbuka kama una matatizo yoyote ya kiafya kama pumu, maradhi ya moyo, mapafu, matatizo ya mifupa, misuli na mengineyo ni vyema ukamuona daktari kwa ushauri kabla ya kuanza kufanya mazoezi haya.FANYA MAZOEZI KWA AFYA BORA!

Sunday, February 9, 2014

Mambo sita (6) ya kukusaidia kuboresha afya yako leo.

1. Punguza kutumia kilevi (pombe) badala yake ongeza kunywa chai, maji na juisi asilia ya matunda. 2. Punguza kula nyama (hasa nyama nyekundu za wanyama waliwao) badala yake ongeza ulaji wa mboga mboga za majani. 3. Punguza kutumia sukari nyingi au kula vyakula vyenye sukari nyingi badala yake ongeza ulaji wa matunda kwa wingi. 4. Punguza utumiaji wa chumvi nyingi au kula vyakula vyenye chumvi nyingi badala yake ongeza utumiaji wa siki (vinegar) 5. Punguza kuwa na wasiwasi au hofu ya aina yeyote ile badala yake pumzisha mwili wako kwa kuongeza ubora wa usingizi wako kwa kulala mahali safi, tulivu, penye hewa ya kutosha na kwa muda wa kutosha. (saa 6 mpaka 8) 6. Punguza kuwa na hasira kila wakati badala yake ongeza kutabasamu na kucheka kwa furaha kila unapofurahishwa.

Saturday, February 1, 2014

Zijue faida za tunda tikitimaji kwa afya njema.

Tikitimaji ni tunda lenye ladha nzuri na tamu sana. Lina maji kwa 92% na sukari kwa takriban 6%. Licha ya kuwa juisi ya tikitimaji au tunda lenyewe hukata kiu kwa haraka bado kuna faida nyingine nyingi za kiafya tunazonufaika kutokana na tunda hili. Je ulikuwa ukijua tikitimaji lina sukari asilia yenye kukupatia nguvu mwilini, vitamin A, C, E, D, niacin na madini kama ya chuma (iron), calcium, magnesium, manganese, potassium, phosphorus, zinc nakadhalika. Faida nyingine ya tunda hili ni kwamba halina mafuta kabisa hivyo ukila tikitimaji huwezi kuongeza mafuta au cholesterol mwilini. Angalia hii video hapa chini yenye maelezo ya namna ya kutengeneza juisi ya tikitimaji na faida za tunda lenyewe. Hebu tuangalie manufaa ya kiafya tunayopata kutokana na tikitimaji. 1. Huepusha saratani. Tikitimaji ni moja ya tunda lenye wingi wa kemikali iitwayo ‘’lycopene’’ ambayo pia inapatikana katika matunda mengine pamoja na mboga za majani. Kemikali hii inaaminika kuwa ni kuzuizi na tiba asilia ya saratani ya tezi dume (prostrate cancer) kwa wanaume. Saratani ya aina hii inazidi kushamiri ulimwenguni hivyo ikiwa wewe ni mwanaume wa shoka na hutaki kuwa mmoja wa wagonjwa wa saratani ya aina hii (prostate cancer) ni vyema ukafanya tikitimaji kuwa kimbilio lako. 2. Hupambana na maambukizi mbalimbali yaletayo magonjwa. Kwa kula tikitimaji unaongeza uwezo wa mwili wako kuwa imara na kujikarabati kwa haraka. Mfano katika ugonjwa wa ngozi, tikitimaji huboresha ngozi yako na kufanya ionekane yenye afya na yenye kunawiri. Hii ni kwasababu tikitimaji lina kemikali iitwayo ‘’amino acid citruline’’ ambayo baadae hubadilisha na kuwa katika mfumo wa kemikali nyingine ‘’arginine’’. Arginine huchochea uzalishwaji wa chembechembe nyeupe za damu ambazo huwa kama kinga katika eneo lenye jeraha. Licha ya hivyo Vitamin C inayopatikana kwenye tikitimaji huongeza kinga ya mwili. Kazi nyingine ya vitamin C ni kuponya vidonda kwakuwa ina uwezo wa kukarabati na kutengeneza sehemu iliyoharibika kwa ugonjwa. Kama wewe una tatizo la vidonda kutopona kwa haraka, tikitimaji pamoja na matunda mengine yenye wingi wa vitamin C ndio chaguo lako. 3. Husafisha figo. Kwa kuwa asilimia kubwa ya tikitimaji ni maji hivyo maji hayo hufanya tunda hili kuwa ni dawa ya asili inayosaidia figo kuondoa taka mwilini kupitia mkojo. Pia tikitimaji husaidia ini kuvunjavunja na kuondoa sumu mbalimbali na hivyo kurahisisha utendaji mzuri mwili kujisafisha na hatimaye kuwa wenye afya njema. 4. Husaidia kudhibiti ongezeko la shinikizo la damu.(High blood pressure) Tafiti mbalimbali zilizofanywa na wanasayansi wa chakula dawa, wamebaini kuwa kemikali zinazopatikana katika tikitimaji ‘’L-citrulline’’ ambayo ina uhusiano wa karibu na kemikali nyingine iitwayo ‘’L-arginine’’ zote mbili kwa pamoja zinaaminika kusaidia kupunguza shinikizo la damu (high blood pressure) na hivyo kuepusha maradhi mengine yanayohusiana na moyo. 5. Huongeza hamu na nguvu ya kufanya mapenzi.(Viagra asilia) Uchunguzi uliofanywa na wataalamu mbalimbali wa afya ukiwemo utafiti kutoka Chuo Kikuu cha Havard Marekani umebaini sio tu kwamba tikitimaji huboresha mfumo wa mzunguko wa damu wa moyo bali hata pia huongeza hamu na nguvu ya kufanya mapenzi kwa wanaume. Kemikali inayojulikana kama ‘’citruline’’ katika tikitimaji inasaidia kuchochea mishipa ya damu ku-relax na kuruhusu damu izunguke kwa ufanisi wake na kuleta muhamko wa uume kama inavyofanya kazi dawa ya kuongeza nguvu ya kufanya mapenzi (Viagra). Tikitimaji pia linaaminika kuongeza nguvu ya mwili kwa asilimia 23%, hii ni kwasababu tikitimaji lina madini ya magnesium ambayo husaidia katika utengenezwaji wa nguvu mwilini (adenosine triphosphate ATP ) na vitamin B6 ambayo huchochea uzalishaji wa hormone ya kukufanya ujisikie mwenye furaha (dopamine hormone). Angalia hii video clip hapa chini upate maelezo kuhusu tikitimaji kama Viagra asilia kutoka kwenye jarida la afya la Havard University. Ndugu msomaji, leo tumeona ni jinsi gani tunda hili la tikitimaji lilivyo na faida nyingi katika miili yetu. Ushauri wangu ni kwamba kuliko kunywa soda au kilevu chenye sukari nyingi ni bora kama ukiweza tengeneza juisi yako mwenyewe ya tikitimaji ukiwa nyumbani kwa manufaa ya afya yako na familia yako kiujumla. NAKUTAKIA AFYA NJEMA!